Published On:Jumamosi, 22 Novemba 2014
Posted by Hisia
Simba yamnasa mdogo wake Msuva
James Msuva ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Wilbert Molandi na Nicodemus Jonas BAADA
ya kumkosa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, Klabu ya Simba
imehamia kwa mdogo wake, James Msuva katika usajili wa dirisha dogo
linalofunguliwa leo.Simba kwa kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Pope, ilitangaza kutoa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo mwenye kasi katika kikosi hicho.Usajili wa dirisha dogo unatarajiwa kufunguliwa leo Jumamosi na kufungwa Desemba 15, mwaka huu ukishirikisha klabu mbalimbali za ligi kuu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, wamefikia hatua ya kumsajili kiungo huyo baada ya benchi la ufundi la timu hiyo ambalo lipo chini ya Mzambia, Patrick Phiri na Selemani Matola kuridhishwa na kiwango chake.
Chanzo hicho kilisema, Phiri ameridhishwa na kiwango kikubwa cha kiungo huyo mwenye kasi anayecheza namba saba kama anayocheza kaka yake Simon baada ya kumuona kwenye mazoezi ya timu ya vijana ya U-20.
“Uongozi umepanga kukutana na mdogo wake Msuva (James) kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya timu hiyo kwa ajili ya kumsajili katika usajili wa dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa kesho (leo).
“James yupo anaichezea timu yetu ya vijana ya U-20, akiwa hana mkataba wa kuichezea Simba, hivyo tumefikia hatua ya kumsajili kwa mkataba na kumpandisha kwenye timu ya wakubwa, hivyo ni baada ya kuridhishwa na kiwango chake ndani ya uwanja.
“Kocha mwenyewe leo (jana) amemuona akiwa anacheza katika kikosi cha vijana cha U-20, amevutiwa naye kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa anauonyesha, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kumsajili,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa Phiri kuhusiana na kiwango cha James, alisema: “Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kucheza, ukiangalia anaweza kukaba, kontroo yake nzuri na anapiga krosi safi, kuhusu kumsajili siwezi kuzungumza hivi sasa.”