Published On:Jumamosi, 4 Oktoba 2014
Posted by Hisia
NANI MTANI JEMBE 2, SIMBA, YANGA WAANZA KUTAMBIANA
Na Mwandishi Wetu
Shindano la ‘Nani Mtani Jembe2’ linalowakutanisha wakongwe wa Soka
hapa nchini Simba na Yanga, limeanza kwa kasi msimu huu, baada ya jana
kuwepo kwa shamrashamra za aina yake katika uzinduzi rasmi uliofanyika
katika viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.
Mashabiki lukuki wa timu hizo na viongozi wao jana walijitokeza kwa
wingi katika viwanja hivyo katika hafla iliyopambwa na makundi
mbalimbali ya timu hizo yaliyokuwa yakitambiana mwanzo mwisho.
Msimu huu wa ‘Nani Mtani Jembe2’ unaoendeshwa na bia ya Kilimanjaro
Premium Lager- wadhamini wakuu wa timu hizo, ulishuhudiwa Simba akianza
vema katika mchezo wa soka baada ya Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji
Said Tully kuwabuziga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa
mashabiki wa Simba na Yanga uliokuwa sehemu ya uzinduzi huo.
Katika mchezo huo wa soka ambao ulionekana kuwa na ushindani mkubwa,
Simba waliwafunga Yanga iliyoongozwa na nahodha wao Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji Mohamed Bhinda huku kwa upande wa danadana Bhinda akimshinda
Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’,huku kwa upande wa
kuvuta kamba mashabiki wa tiu hizo wakitoka sare.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hizo ‘Kaburu’ wa
Simba pamoja na Mohammed Bhinda wa Yanga wote walianza kujigamba
kuhakikisha wanaibuka na kitita cha mil 100 ambacho kimeandaliwa na
Kilimanjaro Premium Lager.
Kaburu alisema, Yanga wameonekana wazi kuanza kushindwa, baada ya
kuwatembezea kichapo cha bao 1-0 na pia kutoka sare ya kuvutana kamba
hasa wakizingatia msimu uliopita wa Nani Mtani Jembe waliwazidi katika
kila idara isipokuwa katika kura zilizopigwa na mashabiki ambapo Yanga
walipigiwa zaidi kura na kuibuka na kitita cha shilingi milioni 98 kati
ya milioni 100.
“Hapa imeonekana tumetoka sare katika kuvuta kamba, ila Yanga kama
mnavyowajua wanapenda ubishi, wamevuta kamba wengi zaidi ya sisi lakini
tumewaachia tu na msimu huu tutahakikisha tunachukua pesa zote na
kuwaachia kifuta jasho tu,’alisema Kaburu.
Naye Bhinda aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuhakikisha
wanaitendea haki Nani Mtani Jembe2 hii ili Yanga iwagalagaze Simba, kwa
kuwa msimu uliopita waliwawaonea huruma Simba na kuwapa nafasi ya
kuwafunga mabao 3-1 baada ya kuona wamezidiwa katika kuvutana.
“Sisi bwana hatuna shida na hawa watani zetu ndio maana tukawaleta
wachezaji kutoka katika kitovu cha soka Brazil na bila ya kuwaleta sisi
Simba wangetoa wapi nafasi ya kuwaona Wabrazil wakisakata kabumbu
Tanzania,”alisema Bhinda.
Alisema kwa kila bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa
milita 500 ambayo mteja atanunua ataona namba maalum na ataandika jina
la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo na atatuma kwenda
namba 15415 na kwa kufanya hivyo atakuwa amepunguza kiasi cha shilingi
10,000 kwenye akaunti ya klabu pinzani na kuiongezea klabu yake kiasi
hicho cha sh. 10,000.
“Msimu huu ni wa kipekee sana maana tumeona bora atakayefungwa siku
ya mechi ya Nani Mtani Jembe walau apate kifuta jasho cha sh mil 5 huku
mshindi akipata milioni 15. Klabu itanufaika, wachezaji watanufaika na
mashabiki watanufaika. Sasa ni kazi kwenu viongozi kuwahamasisha
mashabiki wa timu zenu,”alisema Kavishe.