Vyombo
kadhaa vya habari vimeripoti kuhusu hali ya mgongano kati ya Kamati ya
Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi Tanzania (Tanzania Premier league
Board).
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania linapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 40(11).Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF.
2.Katiba
ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya TFF kutunga kanuni za
uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa
shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa kuendesha
shughuli zake za kila siku.
3.Bodi
ya ligi ni chombo cha TFF kama vilivyo vyombo vingine vikiwemo kamati
mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya ligi sio chombo huru (its not a
legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina mamlaka ya
kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba
ya TFF inatamka kuwa Bodi ya ligi itaheshimu na kufuata maagizo ya
TFF.Maagizo haya yanatolewa na Sekretarieti ya TFF kwa niaba ya kamati
ya utendaji ya TFF.
5.Mwenye
mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF ni Mkutano
Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo kingine cha chini chenye mamlaka
hayo.
6.Kanuni
za mashindano zinaandaliwa na kamati ya mashindano ya TFF na kupitishwa
na kamati ya utendaji ya TFF. Kikao cha kamati ya utendaji
kilichopitisha rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15 kilihudhuriwa
na Mwenyekiti wa bodi ya ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya ligi na pia
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa Bodi
ya ligi na walishiriki kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji
kilichopitisha kanuni za ligi 2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo
wa mapato ya milangoni na ya udhamini.Katiba ya TFF inaagiza hivyo kuwa
Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa pia ni wajumbe wa kamati ya
utendaji ya TFF. Aidha mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi alikuwepo kwenye
kikao hiki cha kamati ya utendaji kama mwajiriwa.
7.
Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa kuendeleza soka la vijana ni uamuzi
uliopitishwa na kamati ya utendaji.Lengo la kuanzishwa mfuko huu ni kuwa
na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka vyanzo mbali
mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa sasa
miradi hii ni:
(a)
Kuanzisha vituo vya kulea na kuendeleza vipaji vya watoto kuanzia miaka
8-17 (sports centres) katika kila mkoa nchini mwetu.Mradi huu ni
mkubwa utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b)
Kuandaa timu ya taifa umri chini ya miaka 12 kwa ajili ya mashindano
ya Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii itaanza kuandaliwa
mwaka huu Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini ya miaka
12. Hii timu itakusanywa na kuwekwa katika shule moja ya bweni ambapo
watalelewa na kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja huku
wanasoma.Tanzania tumeomba kuwa wenyeji wa fainali hizi.
(c)
Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 14 kwa ajili ya michuano ya
awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka
2017.
(d)
Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 17 kwa ajili ya michuano ya
awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 mwaka
2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya mpira wa wanawake na ligi ya taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi
yote hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania haina udhamini
lakini ni lazima ifanyike ili tujihakikishie tunainua mpira nchini
mwetu.Mafanikio ya miradi hii sio tu yatafaidisha na kuimarisha timu
zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko madhubuti la wachezaji mahiri
wa vilabu vyetu vya mpira wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo vikuu vya mapato ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
- Mapato yatokanayo na mechi za ligi zetu madaraja yote
- Mapato yatokanayo na mechi za kimataifa
- Wadhamini
- Serikali kuu kupitia bajeti za Wizara zenye dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
- Wafadhili
- Shughuli mbali mbali za kutunisha mfuko.
Kamati
ya utendaji ya TFF ilimteua Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa
kwanza wa mfuko huu na wajumbe wake ni Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim
Mafuru, Mzee Ayoub Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh Zarina
Madabida. Bw Henry Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko
huu. Imani ya TFF ni kuwa wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika
uongozi wa jamii watatusaidia kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema
shughuli zake.
Upande
wa TFF tumefungua akaunti maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote
zinazokusanywa kama mchango wa TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5
za makato ya fedha za udhamini na ZILE zitokanazo na mfuko wa
jichangie,TFF inatoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania
kuchangia mfuko huu ili utumike kunusuru mpira wetu. Fedha
zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na kanuni za uendeshwaji wa
mfuko huu.
Hitimisho:
Kila
mwanafamilia wa TFF anawajibika kuheshimu na kufuata maelekezo ya
Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama zilivyopitishwa na Kamati ya
Utendaji ya TFF .Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na
fedha za milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni
hizi uko pale pale. Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia utekelezaji wa
maagizo ya Kamati ya utendaji ya TFF mara moja. Mwenye malalamiko
kuhusu kanuni hizi ayalete kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata
Katiba,kanuni na taratibu za Shirikisho.Sote tunajenga nyumba moja
hakuna haja ya kugombea fito.
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Dar es salaam
02/October/2014