Published On:Jumapili, 28 Septemba 2014
Posted by Hisia
“TUMEANGUKA KWA MARA YA PILI, LAKINI NADHANI BADO HATUJAKATA TAMAA”-NAHODHA JOSEPH OWINO
Owino ni beki tegemeo katika safu ya ulinzi ya Simba sc
NAHODHA wa Simba, Mganda, Joseph Owino amesema
wachezaji wa klabu hiyo hawajakata tamaa kwa matokeo waliyopata katika mechi
mbili za ligi kuu soka Tanzania bara.
Simba ilitoka sare ya 1-1 na Polisi Morogoro
katika mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu iliyopigwa jana uwanja wa Taifa, Dar
es salaam.
Katika dakika ya 32 , Emmanuel Okwi aliifungia
Simba bao la kuongoza akimalizia pasi ndefu ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’
kutoka upande wa kushoto wa uwanja, huku mabeki wawili wa Polisi akiwemo
Lulanga Mapunda wakimuacha Mganda huyo atulize mpira kifuani katika eneo
la hatari na kutikisa nyavu.
Katika dakika 50 Danny David Mrwanda alifunga goli
la kusawazisha baada ya mabeki wawili wa Simba, Masoud Nassor ‘Cholo’ na
nahodha Joseph Owino kugongana na kumuacha nyota huyo wa zamani wa Simba
akifunga.
Kabla ya mechi hiyo, Septemba 20 mwaka huu, Mnyama
aliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union katika mechi ya ufunguzi wa ligi
kuu uwanja huo huo wa Taifa.
Kipa
wa Polisi Morogoro, Abdul Ibad akijaribu kuokoa bila mafanikio mpira
ulipigwa na Okwi na hatimaye Simba kuandika bao la kuongoza
Baada ya matokeo hayo, Owino alisema: “Tumeanguka kwa mara ya pili, lakini nadhani bado
hatujakata tamaa. Tutaendelea kujituma zaidi mpaka tupate ushindi”.
“Hakuna makosa, sababu ni kwamba ligi ndio
inaanza, timu zinashindana kupata pointi, lakini tunajipanga kufanya vizuri’.
Simba walianza mechi kwa kutawala safu ya kiungo
ambapo Jonas Mkude alionesha kiwango kizuri. Alitawala dimba la kati, alikuwa
na jeuri, alipiga pasi sahihi na kuipandisha timu juu, lakini mambo
yalibadilika kipindi cha pili.
Mkude alionekana kuchoka, wakati huo huo Piere
Kwizera, Shaaban Kisiga, Emmanuel Okwi waliokuwa mbele yake walishindwa kurudi
nyuma ipasavyo na kuisaidia timu.
Kuhusu safu ya kiungo, Owino amekiri kwamba
haifanyi vizuri, lakini anaamini kocha Patrick Phiri atafanya kazi.
Owino alisema: “Safu ya kiungo haichezi vizuri
sana, lakini mwalimu atafanyia marekebisha na tutacheza vizuri zaidi”.
Wekundu wa Msimbazi watacheza mechi ya raundi ya tatu Oktoba 4 mwaka huu uwanja wa Taifa dhidi ya Stand United.