Published On:Jumapili, 28 Septemba 2014
Posted by Hisia
YANGA YAAMKA, YAIFUNGA GOLI 2 - 1 PRISONS - IKIWA PUNGUFU
Saimon Msuva ameifungia Yanga goli la ushindi
WANAJANGWANI, Dar Young Africans wameitandika 2-1
Tanzania Prisons katika mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara
iliyomalizika jioni hii uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Mabao ya Yanga chini ya kocha Mbrazil yamefungwa
na Andrey Coutinho katika dakika ya 34 na la pili likatiwa kambani na Saimon
Msuva katika dakika ya 69.
Prisons walijipatia goli la kufutia machozi katika
dakika ya 67 kupitia kwa Ibrahim Isaka Hassan.
UCHAMBUZI WA MECHI
Coutinho alifunga goli hilo kwa mpira wa adhabu
ndogo takribani mita 24. Haruna Niyonzima aliwadanganya mabeki wa Prisons kama anataka
kupiga mpira, lakini akamuachia Coutinho aliyepiga shuti, mpira ukadunda karibu
na goli, kipa Mohamed Yusuph akaugusa wakati anajaribu kuokoa, lakini ukazama
ndama ya nyavu.
Dakika ya 38 Beki wa Prisons, Jacob Mwalobo
aliyekuwa na kadi ya kwanza ya njano alioneshwa ya pili na kuzawadiwa nyekundu
na mwamuzi Andrew Shamba kufuatia kumfanyia madhambi Mrisho Ngassa.
Nidhamu mbovu ya ulinzi kwa mabeki wa Prisons ilisababisha
wakafunwga goli hilo. Wakati wameweka ukuta waliacha uwazi na nyuma yao
alisimama Jaja. Coutinho alipiga mpira ukapita katika eneo hilo na kutikisa
nyavu.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza, Yanga walitawala
zaidi mpira hususani safu ya kiungo.
Mbuyu Twite akicheza nafasi ya kiungo wa ulinzi
alishirikiana vizuri na Haruna Niyonzima aliyecheza mbele yake.
Mrisha Ngassa aliyeshambulia kutoka kushoto
alikuwa anabadilika na kucheza winga ya kulia na wakati fulani kuingia
katikati. Hassan Dilunga aliyeanza winga ya kulia aligongeana vizuri na
Niyonzima na mara kadhaa alimuacha beki wake wa kulia Juma Abdul apande juu kuongeza
kasi ya mashambulizi.
Coutinho alicheza vizuri nafasi ya kiungo mshambuliaji,
ingawa kuna wakati alikuwa anapiga pasi mkaa. Jaja kama kawaida yake
hakuonekana sana, kuna baadhi ya mipira alipata na kujaribu kupiga kichwa,
lakini hakufanikiwa kufunga goli.
Edward Charles aliyechukua nafasi ya Oscar Joshua
aliyeumia mechi iliyopita hakuwa na
presha kubwa kwa upande wake, hivyo alipanda zaidi kuongeza mashambulizi kutoka
winga ya kulia.
Hata Juma Abdul naye alipanda zaidi upande wa
kulia kuongeza kasi ya mashambulizi.
Prisons walicheza vizuri, mara kadhaa walipiga
pasi fupifupi, lakini walikosa kasi ya kwenda mbele. Walijikuta wakikaa zaidi
katika eneo lao na kuwapa nafasi Yanga kucheza zaidi safu ya kiungo.
Wajelajela walionekana kukaa nyuma kwasababu
walikuwa wachache. Ngassa alishindwa kufurahia mechi hiyo kwasababu Prisons
hawakutaka kutoka katika eneo la pili.
Kipindi cha pili Yanga walianza kwa kasi kama
kawaida na kulikalia vilivyo dimba la kati.
Dakika ya 55 Dilunga alikwenda benchi na nafasi
yake kuchukuliwa na Hamis Thabit. Dakika ya 57, Marcio Maximo alimtoa Coutinho
na nafasi yake kuchukuliwa na Saimon Msuva.
Kuingia kwa Msuva kuliongeza kasi zaidi ya Yanga.
Dakika ya 61 alitengenezewa pasi nzuri na Niyonzima na kuachia shuti kali ambalo
halikulenga lango.
Licha ya kuwa pungufu, Prisons walijitahidi
kutengeneza nafasi, lakini walikosa mshambuliaji wa kati. Julius Kwanga alipata nafasi kadhaa, lakini
mashuti yake hayakulenga lango.
Dakika ya 67, Ibrahim Isaka Hassan alifunga goli
safi la kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa kutoka winga ya kulia na
kuisawazishia Prisons.
Ibrahim aliruka juu, Yondani na Cannavaro walimuacha
huru kabisa na kipa Dida akajaribu kuokoa mpira huo , lakini hakuwa na la
kufanya.
Kuingia kwa goli hilo, kuliwaamusha Prisons na kuanza
kupanda juu, lakini nidhamu ya ulinzi haikuwa nzuri.
Dakika ya 69 Saimon Msuva alifunga goli la pili
kwa kichwa akimalizia krosi ya Ngassa iliyochongwa kutoka winga ya kulia.
Ngassa kama kawaida aliburuza mpira na kuingiza
ndani, mabeki wa Prisons, Jumanne Elifadhili na Lugano Mwangama walishindwa
kumzuia Msuva.
Licha ya kufunga, Msuva aliongeza kasi ya Yanga
tofauti na mwanzo na hii ilidhihirisha kuwa Maximo hakukosea kufanya mabadiliko
hayo.
Dakika ya 81 Ngassa alipata nafasi ya wazi baada
ya Mwangama kufanya makosa, lakini alipiga shuti lililotoka sentimita chache
kutoka langoni.
Licha ya kuwa pungufu, dakika za lala salama, Prisons walishambulia
lango la Yanga, lakini walishindwa kuwa na mipango ya kupata goli.
Mabeki wa Yanga walilazimika kupigana kufa na
kupona kuokoa jahazi na mpaka dakika 90 zinamalizika, Yanga walikuwa mbele kwa
2-1
Kwa ujumla kipindi cha pili, Prisons ilikuja juu
na kupiga pasi nzuri. Walionekana kuwa na kasi na kuipandisha timu juu.
Kikubwa walikosa nidhamu ya mchezo, baada ya
kusawazisha goli walikubali kupanda zaidi wakati wako pungufu. Ngassa
alikimbizana na beki asiyekuwa na kasi na wakafungwa aina ya goli lilelile
waliloifunga Yanga.
Prisons si timu ya kuichukulia poa. Ina upinzani
wa hali ya juu na timu nyingine zijipange sana.