Published On:Jumatatu, 22 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA NI DHAIFU KUANZIA TIMU MPAKA MCHEZAJI MMOJA MMOJA….WASHUKURU KUPATA SARE YA 2-2 DHIDI YA COASTAL UNION
SIMBA SC chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri
wamehitimisha raundi ya kwanza ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyoanza
septemba 20 mwaka huu kwa kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal
Union katika mechi yao ya ufunguzi iliyopigwa jana uwanja wa Taifa, Dar es
salaam.
Mbali na kipute hicho, jumamosi (septemba 20 mwaka
huu), kulikuwa na mechi sita ambazo zilileta matokeo yasiyotarajiwa kwa baadhi
ya timu.
Wakiongozwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo katika
mechi ya kwanza ya ligi kuu, Yanga walitandikwa 2-0 na Mtibwa Sugar, uwanja wa
Jamhuri mkoani Morogoro.
Mabingwa watetezi, Azam fc walishinda 3-1 dhidi ya
Polisi Morogoro, wakati washindi wa tatu msimu uliopita, Mbeya City fc wakiwa
nyumbani Sokoine waliambua suluhu pacha ya bila kufungana (0-0) mbele ya JKT
Ruvu kutoka Pwani.
Mgambo JKT waliifunga Kagera Sugar 1-0 katika
uwanja wa Mkwakwani Tanga. Ruvu Shootings wakiwa nyumbani kwao mabatini
walifungwa 2-0 na Tanzania Prisons.
Stand United wakiwa kwao Kambarage mkoani
Shinyanga, walikula kipigo cha 4-1 kutoka kwa Ndanda fc.
Kama nilivyosema awali, Simba ndio walihitimisha raundi
ya kwanza hapo jana na leo hii napenda kuuzungumzia kwa kina mchezo huo.
Kwanza kabisa, Simba washukuru kupata pointi moja
kwasababu walicheza hovyo kama timu na kwa mchezaji mmoja mmoja.
Nitawaelezea baadhi ya wachezaji wao nyota ambao
ni Paul Kiongera, Piere Kwizera, Ramadhani Singano ‘Messi’, Shaaban Kisiga ‘Malone’
, Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe.
Kiukweli, wachezaji wote wa mbele hawakufanya vizuri
na ndio maana safu ya ulinzi ya Simba inaonekana mbovu.
Kitaalamu, timu inajengwa kutoka nyuma, maana yake
ni kwamba kila mtu anatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa nafasi yake.
Ili uweze kupata ubora wa safu ya ulinzi, ni pale
idara nyingine zinapotekeleza majukumu yao ipasavyo. Simba kuanzia idara yao ya
kiungo mpaka ushambuliaji, wako hovyo kupita maelezo.
Kwa leo tuzungumzie matatizo ya Simba kuanzia safu
ya kiungo na Ushambuliaji ambayo chanzo chake ni kusajili hovyo hovyo, bila kufuata
utaratibu na mwisho wake wanajikuta wana wachezaji wengi kwenye nafasi moja au
wana wachezaji wengi wenye majukumu yanayofanana.
Kwahiyo wamejikuta hawana namna zaidi ya kuwatumia
wachezaji wanaofanana, yaani ni kama sare tu. Mfano; wewe una mashati 10 na mashati
8 yote ni mekundu, ukivaa yale yale kwa mfululizo, hutaonekana umebadilisha
nguo, bali umevaa nguo ile ile.
Kocha mkuu wa Simba sc, Patrick Phiri
Tukianza na wachezaji waliocheza jana kwenye safu
ya kiungo;
PIERE KWIZERA
Ni mchezaji mzuri, lakini hana maamuzi ya haraka.
Yuko pole pole kwenye baadhi ya ‘Movement’. Kuna wakati yeye ndiye anatakiwa
Kuanzisha ‘movement’ za haraka kwenda kwenye goli la mpinzani, lakini anakosa maamuzi sahihi kwa muda muafaka, pamoja na
kwamba hapotezi pasi.
Kutopoteza pasi sio kigezo. Ni mara mia upoteze
pasi nne kati ya sita ambazo zilitakiwa kufika katika eneo sahihi, kuliko
kutopoteza pasi nne kati ya nne ambazo hazina faida yoyote wala madhara yoyote.
Maana yangu
ni kwamba kama ulitaka kupiga pasi katika eneo sahihi ukakosea, ule mpira bado
utakuwa katika eneo lile lile la hatari na mtu mwingine anaweza kuupitia na
kusababisha madhara. Hii ina faida kuliko kupiga pasi ambayo haina madhara
yoyote.
Uwezo wa Kwizera kufanya maamuzi ni mbovu kabisa. Sijawahi
kumuona akicheza huko nyuma zaidi ya kumuona Simba, labda hiyo sio nafasi yake
sahihi. Nijitolee mfano mimi mwenyewe Shaffih Dauda.
Mwaka 2002 nakumbuka Simba ilikuwa inatafuta
wachezaji wa kusajili pale nje ya uwanja wa Taifa ambapo sahizi pana uwanja
mpya wa Taifa.
Walikuja wachezaji wengi mno kufanya majaribo na
mimi nilienda. Lakini kwenye nafasi yangu ya kiungo nikakutana na mtu mmoja
anaitwa Salim Lyandungu, Yahya Akilimali, William John, Mpandachi na Joel Noel.
Nikagundua kuwa ushindani ni
mkubwa, lakini kwenye safu ya ulinzi kulikuwa na wachezaji wachache akiwemo
Patrick Betweli, Aman Mbarouk, Benito John na Chacha Marwa. Na mimi nikajifanya
beki kwasababu ilikuwa ni rahisi katika nafasi ile. Ulikuwa unapata nafasi ya
kucheza kwa muda mwingi kuliko nafasi ya ushambuliaji au kiungo ambayo
walikuwepo watu wengi sana.
Katika mchujo huo, Benito John na Chacha Marwa hawakufanikiwa,
wakati mimi, Patrick Betweli na Aman Mbarouk tulifuzu majaribo.
Mimi na Mbarouk tulisajiliwa siku moja katika klabu ya Simba
mwaka 2003 na Rais wa Simba wa sasa, Evens Elieza Aveva ndiye alitusainisha
fomu katika Hoteli ya Embassy ambako alikuwa anafanya kazi zamani .
Nilipata nafasi ya kucheza Simba kama beki wakati mimi nilikuwa
kiungo na baadaye nilipopata nafasi, nikataka kucheza nafasi yangu.
Lakini kwa bahati mbaya sikuendelea kucheza mpira wa ushindani
kutokna na sababu zilikuwa nje ya uwezo wangu na badala yake nikajikita katika
masomo.
Nini maana ya mfano huu? Kwizera mimi siwezi
kumlaumu, inawezekana baada ya kuja Simba ndio nafasi iliyopata, yawezekana
kuna nafasi nyingine ambayo anacheza vizuri zaidi. Kwasababu hakuna mtu aliyemuona
kabla, anajikuta anajaribiwa.
SHAABAN KISIGA ‘MALONE’.
Kisiga ni namba 10 na sio namba 8. Ili upate
kiwango cha Kisiga ni pale anapocheza kama mshambuliaji, yaani wacheze
washambuliaji wawili au acheze nyuma ya mshambuliaji, kwa mfano acheze na
Tambwe au nyuma ya Tambwe.
Kwa vile Simba kwenye idara ya ushambuliaji wana
Tambwe, Emmanuel Okwi na Paul Kiongera, Kisiga anarudishwa kucheza namba 8.
Eneo ambalo hawezi kucheza vizuri kama anavyocheza namba 10.
Simba wanashindwa kupata kiwango bora cha Kisiga
kwasababu anacheza eneo ambalo hachezi vizuri. Inatokea hivi kwa sababau lile
eneo analotakiwa kucheza yeye kuna wachezaji wengine, hivyo amembidi atafute
eneo lingine la kucheza na hatimaye kupata namba 8 ingawa sio eneo lake sahihi.
Kwa mfano jana kwenye mechi, Kisiga alikuwa anapiga
pasi vizuri, lakini hakuwa na kasi, alikuwa polepole sana, hakupiga zile ‘killer
pass’ na sababu kubwa ni kutocheza katika eneo lake.
Messi (kushoto) akifanya mambo yake
RAMADHANI SINGANO ‘MESSI’.
Labda jina la Messi linamharibia. Kila mpira yeye
anataka awatie watu njaa, akokote vile anavyotaka. Hata Lionel Messi mwenyewe
wa Barcelona, kuna mipira mingine anapiga pasi moja na huwa hakimbizi kwasababu
anahofia kuchoka.
Uwepo wa Singano uwanjani una faida kwa dakika
chache kwasababu muda mwingi unataka kila mpira unaoenda kwakwe akimbize, na akishapoteza
hawezi kukaba, hawezi kurudi kuisaidia timu kujilinda na matokeo yake
anaigharimu.
Ili Singano
aweze kuisaidia timu, sio kila mpira ukienda kwake aburuze. Wakati fulani aachie
pasi moja moja na akifanya hivyo atampa mtu mwingine nafasi ya kucheza vizuri na
yeye mwenyewe hatachoka.
PAUL KIONGERA
Simba
wamemsajili mchezaji mwenye pancha mwili mzima. Ana majeruhi ya goti na hapa
ndipo unapata madhara ya kujisajiliwa hovyo hovyo tu.
Mchezaji
katoka huko, hamjui historia yake, mnamsajili kishabiki tu kwaajili ya kuwahi siku
ya mwisho ya usajili ‘Deadline’. Matokeo yake mnapata mchezaji mwenye majeruhi.
Mimi nimemfuatilia katika mechi za Simba, mchezaji huyu ana jeraha ambalo hawezi kupona leo wala
kesho.
Kama unabisha, baada ya kuumia katika mechi ya jana, ukiangalia
lugha ya mwili ‘Body language’, yule mchezaji ana majeraha na Simba wamemsajili
akiwa na majeraha.
Wazungu sio wajinga wanapofanya vipimo vya afya,
wanataka kujua kama mchezaji ni mzima. Simba wangekuwa makini wasingesajili
mchezaji mwenye pancha. Hapa wamepata hasara na hatakuja kuitumikia timu vile
inavyotakiwa.
EMMANUEL ANORD OKWI
Huyu ndiye mchezaji aliyecheza chini ya kiwango
mno licha ya kutoa pasi moja iliyozaa goli alilofunga Tambwe.
Okwi (kulia) akimtoka beki wa Coastal Union
Okwi amekwisha, huo ndio ukweli, labda inabidi awe
na mazoezi maalumu “Special Training’ kwaajili ya kurudisha kiwango chake.
Yaani Okwi yule wa 5-0 na yule wa Setif, sio huyu wa sasa hivi.
Simba walijua fika kuwa mchezaji huyu alikuwa
hachezi, alikuwa kwenye matatizo na klabu yake. Wamekurupuka kumsajili na kumpa
mechi, lakini kiukweli hana ‘Match fitness’ hata kidogo, watake wasitake,
ndivyo ilivyo.
Haikatazwi kumsajili mchezaji ambaye hana ‘fitness’
kwasababu unajua umuhimu wake, lakini asiharakishwe kucheza. Ni bora wakacheza
watu wengine ambao tayari wameshajiandaa kwa msimu.
Kwani Okwi kacheza Simba lini? Si kasajili juzi
juzi tu dakika za mwisho? Alikuwa anafanya mazoezi wapi? Wamemsajili kutoka
timu gani? Kafanya wapi maandalizi ya kabla ya msimu?
Labda viongozi watukumbushe. Okwi hana ‘fitness’ ,
Simba wanatakiwa kumtengenezea program maalumu
ili kurudisha kiwango chake, lakini kama wanataka kuwafariji mashabiki wao basi
waendelee kumtumia. Lakini haitakuwa na maana kama timu itaathirika kiufundi na
kimbinu na wakati wanagundua watakuwa wameshachelewa.
Okwi alikuwa mchezaji wa kutegemewa katika timu ya
taifa ya Uganda, lakini leo hii hayupo. Na tatizo ni kwamba hana ‘Match fitness’
na kilichochangia ni kutocheza mpira. Sasa Simba wanapata wapi ushujaa wa
kumchezesha? Au kwasababu ni Okwi? Kwanini wasianze na wachezaji waliokuwa nao
katika maandalizi ya kabla ya msimu na yeye akacheza na wenzake baadaye? Okwi
hakuna kitu pale.
HARUNA CHANONGO (pichani kushoto)
Huyu ni mchezaji mzuri, lakini mambo yetu ya
U-simba na U-yanga yamemharibu. Moja ya wachezaji ambao wangekuwa wamefika
mbali mpaka sasa hivi ni Chanongo.
Kutokana na
tetesi za kuuza mechi, mfano ile ya Simba na Yanga ambayo alisimamishwa kwa
madai kuwa amekula mlungula au rushwa, Chanongo ameathirika sana.
Ukiangalia uchezaji wake, Chanongo amepungua.
Alikuwa anachukua mpira anazama ndani katika eneo la hatari, lakini leo hii
kila sehemu akienda anaogopa, anadhani akikosea watu watasema ameuza mechi.
Kwahiyo anatafuta njia rahisi ya kujisafisha. Kila
mpira anataka ageuke na kupiga pasi nyuma ili asipoteze, lakini Chonongo kama angecheza
Chanongo yule yule wa Bank ABC, Chanongo yule wa msimu uliopita, angekuwa
mchezaji mzuri, lakini kutokana na mambo ya U-simba na U-yanga. Wameshindwa kulea
kipaji cha mchezaji. Chanongo ni muoga, anaogopa kuingia, anajihami kukosea.
Chanongo mdogo wangu ninayekujua mimi sio.
Usiogope maneno ya watu, cheza mpira, mabeki wawili wafuate, ingia kwenye
boksi. Leo hii mbona sikuoni ukiingia kwenye boksi, unageuka na kurudi nyuma,
kulikoni?
AMISSI TAMBWE
Mchezaji wa mpira wa miguu ili akamalike anahitaji mambo manne. Utimamu
wa mwili, Ufundi, mbinu na Saikojolia.
Kama mchezaji ana vitu vitatu vya kwanza, lakini
kisaikolojia hayuko vizuri, hivyo vingine ni kazi bure.
Kisaikolojia, Tambwe hayuko vizuri kwasababu yeye
alikuwa Wayne Rooney wa Simba, lakini ghafla kafanywa kama wachezaji wale wale
waliokuja kufanya majaribio na wamesajiliwa.
Zile taarifa
za kusema jina lake lilitakiwa kukatwa ili asajiliwe Okwi anazo.
Binadamu yeyote yule hawezi kuwa sawa kisaikolojia. Sasa hivi kwenye timu
anapoona yeye ni chaguo la tatu mbele ya Kiongera, na Okwi, halafu akikumbuka
kuwa yeye ndiye mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, kisaikolojia hawezi kuwa
sawa.
Lakini
pamoja na hayo yote, nampongeza Tambwe kwasababu amebaki kuwa Tambwe yule
yule na alifunga goli. Kama Simba wangetengeza nafasi kwa kumuamini yeye angewafungia
magoli, lakini kwa staili hii ya kuonesha hawamuamini na kumfanya kama mchezaji
wa ziada, basi wanampoteza na maisha yake yataishia hapo.
Tambwe bado ndiye mchezaji hodari wa Simba, lakini
kwasababu ya kasumba ya viongozi kupenda wachezaji waliowasajili, matatizo
hujitokeza.
Kwa mfano uongozi ulioingia madarakani, kuna
wachezaji wapya wamewasajili na wanaamini wale waliowakuta sio wachezaji. Watake
wasitake, Amissi Tambwe ndiye mshambuliaji wa Simba.
Kwasababu wachezaji wengine hawakucheza vizuri
kama nilivyoeleza, ubora wa Tambwe haukuonekana. Lakini pale Okwi alipopiga
pasi, iliona namna Tambwe alivyokaa katika nafasi na kufunga goli?, huyo ndiye
Tambwe tunayemjua sisi.
Kuanzi sehemu ya nyuma, Simba timu yao haiko vizuri
kabisa. Wakae chini wajipange, panapo majaaliwa, Mungu atawasaidia.
Jumatatu njema!
Chanzo: shaffihdauda.com