Published On:Alhamisi, 25 Septemba 2014
Posted by Hisia
MECHI YA SIMBA NA YANGA OKTOBA 12 YAPEPERUKA - TFF yapangua ratiba
TIMU
ya taifa – Taifa Stars imesogeza mbele mechi ya watani wa jadi – Simba
na Yanga kufuatia kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) ambayo itaikutanisha Stars na Benin Oktoba 12.
Awali
tarehe hiyo ndiyo ilikuwa imepangwa kwaajili ya mechi ya Simba na Yanga
kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini badala yake sasa
uwanja huo na siku hiyo ya Oktoba 12 itakuwa ni maalum kwaaji ya mchezo
wa kirafiki wa Taifa Stars na Benin.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kwa niaba ya Katibu Mkuu Shirikisho la Mpira Wa Miguu Tanzania, mechi hiyo ya Stars itaanza saa 10 alasiri.
Aidha, taarifa hiyo imesema programu
ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya
mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa
ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu
hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Kutokana
na mechi hiyo, ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inafanyiwa
marekebisho madogo. Marekebisho hayo ikiwemo pia tarehe mpya ya Simba na
Yanga, yatatangazwa kesho (Septemba 26 mwaka huu).