Published On:Ijumaa, 26 Septemba 2014
Posted by Hisia
ANDREY COUTINHO, JERRYSON TEGETE KAMILI GADO KUIVAA PRISONS....
KIKOSI cha timu ya Young Africans kitashuka dimba
la Uwanja wa Taifa siku ya jumapili kupambana na Wajelajela, Timu ya Jeshi la
Magereza,Tanzania Prisons kutoka jijini
Mbeya ikiwa ni mchezo wa pili wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania bara msimu wa 2014/2015.
Akiongea na tovuti
rasmi ya klabu leo mara baada ya mazoezi, kocha mkuu wa Young Africans Mbrazil
Marcio Maximo amesema vijana wake wako fiti kuelekea mchezo huo wa siku ya
jumapili huku wakiwa wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu.
Maximo amesema baada
ya kupoteza mchezo wa awali dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar, kikosi chake
kimekua kikiendelea na mazoezi kila siku katika uwanja wa shule ya sekondari
Loyola huku wakiyafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo wa
awali.
Kuhusu timu ya
Tanzania Prisons, Mbrazil Maximo amesema anatambua walishinda mchezo wa awali
dhidi ya Ruvu Shooting hivyo wana morali bado ya kuendeleza ushindi siku ya
jumapili, lakini pia kikosi chake kipo fiti kusaka pointi tatu muhimu.
Aidha Maximo amesema
habari njema kwa wana Yanga ni kurejea dimbani kwa kiungo Andrey Coutinho
pamoja na mshambuliaji Jerson Tegete ambao wanatarajiwa kuonekana kwenye mchezo
huo na kuhakikisha wanaisaidia timu yao kupata ushindi.
Wachezaji
watakaoukosa mchezo wa siku ya jumapili ni Oscar Joshua na Hussein Javu ambao
wote ni majeruhi, wakisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, na jumatatu
wanatarajiwa kuanza mazoezi mepesi baada ya kuwa kwenye matibabu chini ya
usimamizi wa daktari wa timu Dr Suphian Juma.
Marcio Maximo amewaomba wapenzi, washabiki, wanachama na wadau wa soka kwa ujumla kujitokeza kwa wingi siku ya jumapili katika mechi dhidi ya Prisons kuja kuwapa sapoti vijana na kuwashangilia muda wote wa mchezo.