Headlines
Published On:Jumapili, 28 Septemba 2014
Posted by Hisia

NIDHAMU YA MCHEZO ITAWAEPUSHIA KIPIGO KAGERA SUGAR MBELE YA JKT RUVU LEO!

Kikosi cha JKT Ruvu kilichoanza dhidi ya Mbeya City fc uwanja wa Sokoine Mbeya na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana (0-0)

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
JKT Ruvu wanaikaribisha Kagera Sugar katika mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara inayopigwa leo jioni uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi za raundi ya kwanza, septemba 20 mwaka huu, JKT Ruvu walitoka 0-0 na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakati Kagera Sugar walipoteza 1-0 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
Mechi hii itakuwa ngumu kwa timu zote kwasababu hazikupata matokeo mazuri katika mechi ya kwanza.
Bora hata JKT Ruvu waliambulia pointi moja kuliko Kagera Sugar waliopoteza kila kitu.
Kocha wa Kagera Sugar, Mganda, Jackson Mayanja anahitaji kushinda mechi hii, lakini anatakiwa kufanya kazi ya ziada sana.
JKT Ruvu wameimarika chini ya kocha wao Fred Felix Minziro. Sio wale wa msimu uliopita. Wamesajili vizuri na maandalizi yao yalikuwa mazuri.
Walisajili wachezaji wazuri kama, Haruna Shamte, Jabir Aziz na Kipa Jackson Chove Mandanda.
Kipa huyu hana uhakika wa kucheza kwasababu alipata majeruhi ya kichwa katika mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City fc na Rais wa TFF, Jamal Malinzi alitoa amri ya kutochezeshwa mpaka JKT Ruvu wapeleke vipimo vya daktari.
FIFA wana sheria yao kuwa mchezaji anapopata majeruhi ya kichwa, anatakiwa kupimwa kwanza ili kujua kama hana matatizo makubwa kabla ya kuruhusiwa kucheza.
Wachezaji wa Kagera Sugar wakifanya mazoezi

Mbali na nyota hao, Minziro aliongeza nguvu zaidi ya kikosi chake kwa kusajili wachezaji wengi wapya na kuwapeleka wengi kucheza kwa mkopo JKT Oljoro na wengine kama Hussein Bumu kustaafu soka.
Ni JKT Ruvu mpya kabisa. Ina nidhamu ya mpira na mipango ya kushinda.
Katika mechi dhidi ya Mbeya City fc walishambuliwa sana, lakini nidhamu bora ya ulinzi iliwafanya wasifungwe.
Timu ilishambulia, ilijilinda vizuri na kuepuka kufungwa. Makocha duniani kote wanapenda kufundisha vitu vitatu muhimu. Kujilinda, kucheza mpira na kushambulia.
Ubora wa timu huanza nyuma. Kama una beki nzuri na viungo wazuri, unaweza kufunga na usifungwe.
Minziro ni mwalimu anayependa kucheza soka la kuvutia. Hata JKT Ruvu wameonekana kubadilika. Wanacheza mpira, wanapigiana pasi na wana nidhamu ya mpira.
Kwa mazingira haya, Kagera Sugar wanahitaji kuingia na mbinu kali za kuwafunga Maafande hao.
Msimu uliopita, Kagera walikuwa bora zaidi ya JKT Ruvu, lakini rekodi hiyo isiwadanganye, timu imekuwa mpya msimu huu.
Nidhamu ya mchezo itawaokoa Kagera Sugar, lakini kwa JKT Ruvu niliyoitazama dhidi ya Mbeya City, wanaweza kuangukia pua.

Mechi hii ni ngumu, lakini nawapa asilimia nyingi JKT Ruvu kushinda. Kagera wanaweza kushinda pia, lakini sioni nafasi yao kwa kuzingatia kiwango walichoonesha kule Tanga wakichapwa 1-0 na Mgambo JKT.

About the Author

Posted by Hisia on 9/28/2014 07:11:00 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

By Hisia on 9/28/2014 07:11:00 AM. Filed under . Follow any responses to the RSS 2.0. Leave a response

0 comments for "NIDHAMU YA MCHEZO ITAWAEPUSHIA KIPIGO KAGERA SUGAR MBELE YA JKT RUVU LEO!"

Leave a reply

    Blog Archive