Published On:Alhamisi, 25 Septemba 2014
Posted by Hisia
MURAGE KABANGE - "TUMEPOTEZA MECHI YA KWANZA, HATUTAKI KUPOTEZA YA PILI"
KAGERA SUGAR imejificha jijini Dar es salaam
kujiwinda na mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara
itakayopigwa jumapili (septemba 28 mwaka huu) dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Azam
Complex, Chamazi.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange
amesema baada ya kupoteza mechi ya kwanza 1-0 dhidi ya JKT Mgambo katika uwanja
CCM Mkwakwani jumamosi iliyopita, hawatakuwa tayari kuacha pointi tatu mbele ya
maafande hao wa Pwani.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na
ubora wa kikosi cha Fred Felix Minziro kilichotoka suluhu pacha ya bila kufungana
na Mbeya City fc katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu jumamosi iliyopita uwanja
wa CCM Sokoine, Mbeya.
JKT Ruvu ilionekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu
ya mchezo, na Minziro alisema timu yake ilicheza vizuri na sasa wanaipigia
hesabu Kagera Sugar.
Lakini Kabange wa Kagera Sugar alisema: “Tumerudi
na tuko hapa Dar es salaam tangu jumatatu. Vijana wanajitahidi katika mazoezi
na tutahakikisha tunafanya vizuri.”
“Mechi iliyopita tulijikwaa kidogo, tulipata
nafasi za kufunga pamoja na penalti, lakini hatukufanikiwa kufunga.
Tunarekebisha matatizo ya kikosi chetu na tunaamini mechi ijayo dhidi ya JKT
Ruvu tutafanya vizuri.”
“Mpira umebedilika duniani kote, unaweza kushinda mahali popote, tunajua ugumu wa wapinzani wetu, lakini tumejipanga. Tumepoteza mechi ya kwanza na hatutaki kupoteza mechi ya pili”.