Published On:Jumamosi, 27 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA YATOKA SARE YA GOLI 1 - 1 DHIDI YA POLISI MORO - TAIFA LEO
Emmanuel Okwi amefunga goli lake la kwanza msimu huu
WEKUNDU wa Msimbazi Simba sc wamelazimishwa sare
ya 1-1 dhidi ya Polisi Morogoro katika mchezo wa pili wa ligi kuu soka Tanzania
bara uliomalizika jioni hii uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Hii ni sare ya pili kwa Simba kwani mchezo wa
ufunguzi wikiendi iliyopita waliambulia pointi moja kufuatia sare ya 2-2 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga
katika uwanja huo huo.
Simba walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza
kupitia kwa Mganda Emmanuel Anord Okwi katika dakika ya 32, wakati Danny David Mrwanda
aliisawazishia Polisi Moro bao hilo katika dakika ya 50 ya kipindi cha pili.
UCHAMBUZI WA MECHI
Kipindi cha kwanza mpira ulianza pole pole, Simba
wakitawala zaidi safu ya kiungo chini ya kiungo wa ulinzi aliyerejea baada ya
kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeruhi, Jonas Mkude.
Licha ya kutocheza kwa muda mrefu, Mkude alionesha
kiwango kizuri katikati ya uwanja, alipiga
pasi sahihi, alitawala mpira kwa kugusa na kuachia na kuisukuma timu kwenda
mbele, huku Piere Kwizera aliyepandishwa juu kidogo akijitahidi kuisaidia timu.
Shaaban Kisiga aliyecheza nyuma ya Tambwe alicheza
vizuri, alipiga pasi kama afanyavyo akiwa katika nafasi hiyo, lakini hakuwa
katika kiwango chake kilichozoeleka.
Simba walifika zaidi golini kwa Polisi na mpaka
kipindi cha kwanza kinamalizika walipata kona tano kwa tatu. Amissi Tambwe na
Emmanuel Okwi walikosa nafasi kadhaa za kufunga.
Dakika ya 26 Okwi alikosa nafasi ya wazi kabisa akidhani
ameotoa na mpira ukaokolewa na kipa na kuwa kona ambayo ilizalisha hatari
langoni mwa Polisi, lakini Simba wakakosa tena nafasi hiyo.
Okwi alifuta makosa yake na kuandika bao la
kuongoza katika dakika ya 32 akimalizia pasi ndefu ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’
kutoka upande wa kushoto wa uwanja, huku
mabeki wawili wa Polisi akiwemo Lulanga Mapunda wakimuacha Mganda huyo atulize mpira kifuani katika eneo la
hatari na kutikisa nyavu.
Kilichoonekana kubadilika kwa Simba tofauti na
mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union waliyotoka sare ya 2-2 ni utulivu mkubwa
sehemu ya kiungo. Mkude amerejea na mchango wake umeonekana dhahiri.
Lakini mechi hii mpaka dakika 45 za kipindi cha
kwanza zinamalizika, haikufikia hata nusu ya ubora wa mechi iliyopita.
Polisi Moro walianza mechi kwa kulinda zaidi eneo
lao na hawakufanikiwa kupiga shoti lolote lililolenga lango.
Waliweka mpango mkakati wa kumkaba Okwi na Tambwe
na kila mpira ulipofika walikuwa mabeki watano dhidi ya wachezaji watatu wa
Simba.
Haikuwa rahisi kwa Simba kupenya ngoma ya Polisi,
lakini baada ya kufungwa bao la kwanza walifunguka na kusogea mbele na wakapata
kona moja.
Danny Mrwanda aliyesimama mbele alionekana
kupambana, lakini alikuwa na kitu kama ‘jaziba’. Aliingia kwenye mivutano mara
kadhaa na mabeki wa Simba.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza
zinamalizika, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha kwanza Polisi walianza vizuri mechi na
kudhihirisha kocha wao Adolph Rishard amewaelekeza nini cha kufanya.Walionekana
kuwa na nguvu kubwa wakipanda juu na kushambulia.
Katika dakika 50 Danny Mrwanda alifunga goli la
kusawazisha baada ya mabeki wawili wa Simba, Masoud Nassor ‘Cholo’ na nahodha
Joseph Owino kugongana na kumuacha nyota huyo wa zamani wa Simba akifunga.
Cholo aliteguka mkono na kutolewa kabisa uwanjani
na Patrick Phiri akalazimika kumuingiza Willium Lucium ‘Gallas’.
Dakika ya 58 kwenda 59 Ramadhani Singano ‘Messi’
alimmegea pande nzuri Shaaban Kisiga ambaye alimtafuta Tambwe, lakini Mrundi
huyo akaukosa na mpira kunyemelewa na Okwi aliyejaribu kupiga, lakini mabeki
wakatoa mpira na ikawa kona.
Okwi alichonga kona nzuri kutoka wingi ya kushoto ,
Tambwe akaruka juu na kupiga kichwa murua, lakini mpira uligonga mtambaa panya.
Mechi iliendelea kuwa na kasi, lakini Simba
walikufa katikati na pengine Mkude alipungua kasi kwasababu hajacheza muda
mrefu.
Simba wakishika mpira walikuwa wazuri, lakini
wakipoteza walikuwa na mipango mibovu na hatimaye kujikuta wakishambuliwa mara
kadhaa.
Okwi, Kisiga na Kwizera hawakuweza kurudi nyuma
kiufanisi kuisaidia timu inapopoteza mpira, wakati huo huo Mkude akiwa hana
kasi ya kutosha nafasi ya kiungo wa ulinzi.
Phiri aliliona hilo haraka na kuamua kumtoa Kisiga
na nafasi yake kuchukuliwa na Amri Kiemba ‘Baba wawili’.
Pamoja na kuingia kwa Kiemba, Simba walionekana
kutanua sana katikati wakishika mpira, lakini wakipoteza walikuwa wanashindwa
kurudi kuzuia mipira kutokea sehemu hiyo muhimu ya timu.
Dakika ya 74 Tambwe alitolewa na nafasi yake
kuchukuliwa na Elias Maguli.
Dakika ya 89 uliingizwa mpira wa hatari langoni
mwa Simba, Suleiman Kassim ‘Selembe’ alipiga kichwa, mpira ukagonga mwamba na kipa
Casillas akaudaka mpira huo.
Dakika za mwisho, Simba walifika langoni mwa
Polisi, lakini Amri Kiemba na Singano walishidnwa kutegua mtego wa kuotea.
Kiujumla Simba wameendelea na tabia yao ya kuanza
mechi vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili wanalowa kwa
kiasi fulani.
Licha ya kujitahidi kushambulia, lakini Simba
walikufa safu ya kiungo nadhani ilitokana na Mkude kuchoka kwa kiwango fulani.
Polisi Morogoro walifunguka na kucheza mpira
mkubwa kipindi cha pili. Wangekuwa makini wangefunga magoli kadhaa.
Kocha Phiri analazimika kuwarudisha wachezaji darasani, kuwatafutia kasi ya dakika 90 wachezaji wake na kurekebisha safu ya kiungo.