Published On:Alhamisi, 25 Septemba 2014
Posted by Hisia
MBEYA CITY FC YATAKIWA KUOMBA MECHI ZA KIRAFIKI MALAWI
Balozi wa Tanzania Nchini Malawi,
Patrick Tsere, mwenye suti katikati akipokea picha ya ya wachezaji wa Mbeya
City toka kwa wanahabari wa mkoa wa Mbeya
TIMU ya mpira wa miguu
ya Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetakiwa kupeleka
mwaliko wa kuomba Timu za kujipima nguvu kutoka nchini Malawi ili
kuimarisha ujirani mwema kupitia sekta ya michezo.
Hayo yalibainishwa na
Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Patrick Tsere, alipokuwa akizungumza na
Waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya waliofanya ziara ya kimafunzo nchini
Malawi na kumkabidhi picha ya Wachezaji wa Mbeya City kwa lengo la kuitangaza
timu hiyo kimataifa.
Balozi Tsere alisema atalichukua
jukumu la kuitangaza Mbeya City kama moja ya kazi yake nchini Malawi isipokuwa
suala muhimu ni uongozi wa timu hiyo kutuma barua za maombi ya kuzialika timu
kutoka Malawi ili kucheza michezo ya kirafiki hali ambayo itachangia kuimarisha
ujirani mwema na ushirikiano uliopo.
Suala na kuinadi Mbeya
City limetokana na maombi ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya
kwa waandishi wa Habari waliofika Ofisini kwake kumuaga katika safari ya
kuelekea nchini Malawi ambapo alisema hivi sasa Mbeya city inajulikana kila
kona nchini hivyo inabidi itangazwe kimataifa.
Hata hivyo Waandishi
hao wakiwa nchini Malawi, mbali na kumkabidhi picha Balozi pia walipata
kuzungumza na Waziri wa Habari, Utalii na utamaduni wa Malawi, Kondwani
Nankhumwa, ambaye alipogusiwa kuhusiana na Mbeya city alisema haina tatizo
atalifikisha kwa Afisa anayehusika na michezo.
Alisema mbali na
kulifikisha suala hilo kwa afisa anayehusika pia alisema ni jukumu la Mbeya
City kupeleka barua ya mwaliko kwani kuna timu nyingi ambazo zinaweza kupambana
na Mbeya city katika michezo ya kirafiki.
Na Mbeya
yetu
|