Published On:Jumapili, 28 Septemba 2014
Posted by Hisia
YANGA ‘WAKITAITIWA’ SAFU YA KIUNGO..JAJA ATAISHIA KUZUNGUKA TU!
Jaja alishindwa kufunga dhidi ya Mtibwa na kwa bahati mbaya alikosa mkwaju wa penati
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
YANGA SC wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa
2-0 katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu soka Tanzania bara, septemba 20 mwaka
huu uwanja wa Jamhuri Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, leo jioni wanaikaribisha
Tanzania Prisons katika mtanange wa raundi ya pili uwanja wa Taifa, Dar es
salaam.
Prisons wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na
kumbukumbu ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting waliopata katika mechi ya
ufunguzi iliyopigwa wikiendi ya septemba 20 mwaka huu uwanja wa Mabatini,
Mlandizi, mkoani Pwani.
Kocha mkuu wa Yanga, Mbrazil, Marcio Maximo bila
shaka atatumia mbinu ya kushambulia zaidi kwa lengo la kufunga mabao mengi,
lakini akijaza viungo wengi kwa ajili ya
kujilinda.
Maximo hupendelea kuchezesha viungo wengi na
kumsimamisha mshambuliaji wa Kibrazil, Genilson Santos Santana ‘Jaja’. Ni kocha
ambaye huwa hahitaji mabao mengi, anapenda kufunga goli moja au mawili, halafu
anaimarisha ulinzi ili kuvuna pointi tatu.
Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba
washambuliaji wawili, Mtanzania, Jerryson John Tegete na Andrey Coutinho
wamerejea baada ya kushindwa kucheza mechi iliyopita kwasababu ya majeruhi.
Coutinho kipenzi cha mashabiki wa Yanga ana
asilimia ‘200’ za kuanza katika mechi ya leo kuliko Tegete na maana yake
atacheza nyuma ya Jaja.
Coutinho (kulia) yako fiti kuivaa Prisons leo
Kutokana na aina ya uchezaji wake, amekuwa mwiba
kwa mabeki wa timu pinzani kwasababu ana vitu vingi. Anaweza kupiga chenga,
anamiliki mpira, anapiga pasi za mwisho, ana mashuti ya mbali na kasi nzuri.
Itakuwa mechi yake ya kwanza ya ligi kuu, lakini
alishaonesha uwezo mzuri kwenye mechi za kirafiki wakati wa maandalizi ya kabla
ya msimu.
Kama ataendelea kuwa katika ubora wake, mabeki wa
Prisons wanatakiwa kujipanga kuhakikisha hawampi nafasi ya kucheza atakavyo. Wakimuachia,
anaweza kuwafunga au kumtengenezea nafasi Jaja.
Jaja alianza msimu kwa kufunga mabao mawili kwenye
mechi ya ngao ya jamii dhidi ya Azam fc Yanga ikishinda 3-0 . Alitukuzwa na
mashabiki wa Yanga na kugeuka kuwa habari ya mjini. Lakini hakufanikiwa kufunga
kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kwa bahati
mbaya zaidi alikosa penalti katika mechi hiyo, hivyo leo anahitaji
kufuta makosa hayo na kurudisha imani kwa mashabiki wa Yanga.
Jaja ataingia uwanjani akiwa na wazo moja tu la
kutikisa nyavu. Uchezaji wake haukubaliki kwa mashabiki wa Yanga, lakini mabao
mawili aliyoifunga Azam yalimpa sifa kubwa, hususani goli la pili ambalo
alipiga mpira kiufundi mno.
Tegete (kushoto) amerejea tayari kwa kuanza kazi
Jaja anacheza ‘kivivu’, hana uwezo wa kupiga rangi mpira,sio mkali wa
kumiliki mpira, Jaja hana kasi uwanjani, lakini ni mtu hatari sana anapofika
golini kama atapigiwa pasi za mwisho.
Katika mechi ya Mtibwa Sugar, hukugusa sana mpira,
lakini pasi nne alizopigiwa almanusura afunge magoli. Tatu alipiga vichwa vya
hatari, lakini kipa wa Mtibwa, Said Mohammed aliendelea kuwa katika ubora wa
kuokoa hatari hizo.
Moja alifunga goli, lakini mwamuzi alikataa akidai
nahodha wa Mtibwa, Shaaban Nditi alishika kwa mkono mpira kabla na akatoa
penalti ambayo Mbrazil huyo alikosa. Kwa takwimu hizo, unaweza kuona jinsi gani
Jaja anaona lango na anajua kujipanga maeneo sahihi.
Kama Prisons wanahitaji kushinda leo au kutoa
sare, wanahitaji kuzuia mipira ya Yanga kuanzia katikati.
Uhai wa Jaja unatokana na viungo wa kati na
pembeni. Kama Mrisho Ngassa ataanza winga ya kushoto na Saimon Msuva winga ya
kulia, halafu kiungo mchezeshaji akaanza Haruna Niyonzima na kiungo
mshambuliaji (namba 10 ) akaanza Coutinho na bahati mbaya wakawa katika kiwango
chao, nina uhakika Jaja atafunga.
Bila shaka Mbuyu Twite atacheza nafasi ya kiungo
wa ulinzi, yaani mbele kidogo ya Yondani na Cannavaro. Nyota huyu amekuwa
akifanya vizuri eneo hili na mipira mirefu inayorusha, inawasaidia sana Yanga
kutengeneza hatari kwa wapinzani.
Mrisho Ngassa (kulia) ni mtu hatari sana na anapaswa kuchungwa na Prisons
Yanga wamekuwa bora zaidi katikati japokuwa staili
ya uchezaji wa Niyonzima imebaki kuwa ile ile. Anapenda kugeuka na kupiga pasi
za nyuma , anapenda kupiga chenga na wakati fulani hupunguza kasi ya kupanga
mashambuliaji.
Niyonzima ndivyo alivyo, kumbadilisha sio rahisi,
lakini ni mtu anayeweza kupiga pasi nzuri na zikafika maeneo sahihi. Kama
hatachungwa leo, anaweza kutengeneza hatari kubwa kwani anaweza kuwapa mipira
mizuri akina Ngassa, Msuva, na Coutinho ambao watampa pasi za mwisho au krosi nzuri
mshambuliaji wa kati, Jaja au kufunga wenyewe.
Prisons wanatakiwa kuja na mpango mkakati wa
kuzuia mipira yote ya katikati. Staili ninayoona inaweza kuwasaidia ni
kutowafanya Yanga wawe huru kucheza mpira wao.
Wanatakiwa kukaba mtu kwa mtu na kurudi wengi nyuma
kama timu. Haitawafaa kupaki basi, lakini timu inatakiwa kukaba kwa pamoja.
Prisons wana marali kubwa baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting
Wakipoteza mpira wanatakiwa kurudi wote nyuma ili
kuweka ngome imara ya ulinzi. Kama wataamua kupaki basi moja kwa moja itakuwa
hatari zaidi kwao kwasababu watawaruhusu Yanga kukaa zaidi katika eneo lao.
Ikitokea hivyo, watashambuliwa sana na wanaweza
kujikuta wanapoteza umakini na hatimaye kufungwa magoli mengi.
Mfumo wa kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza
unaweza kuwasaidia zaidi Prisons. Lakini kama wataingia na mfumo wa kucheza
mpira wa wazi (open football), naamini itakuwa ngumu kwao kutokana na mazingira
halisi ya Yanga.
Nina uhakika Yanga watapiga mpira mwingi na wana
hasira za kuanza vibaya, watashambulia sana, lakini hiyo itakuwa faida kwa
Prisons kama watatumia mashambulizi ya kushitukiza.
Kama watapiga mipira mirefu inaweza kuwasaidia
kwasababu Yanga wana tatizo la kujisahau. Kama wana mpira basi wanauchezea
sana, lakini wakipokonywa na kukimbizwa kwa mipira mirefu, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Yondani wanajikuta katika wakati mgumu. (kumbuka mechi na
Mtibwa).
Inawezekana Maximo amerekebisha tatizo hilo, lakini
mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, wanaweza kufanya makosa tena. Hivyo Prisons
wajiandae.
Mpira umebadilika, timu yoyote inaweza kupata
matokeo nyumbani na ugenini.
Prisons walishinda ugenini dhidi ya timu ngumu ya Ruvu
Shooting. Hii imewaongezea morali kubwa . Wanaweza kushindana na kupata matokeo
mazuri.
Polisi Morogoro
walicheza vizuri mno jana. Waliinyanyasa Simba hususani kipindi cha pili
na kuambulia sare ya 1-1. Wengi waliwachukulia poa, lakini wakaonesha kuwa wanaweza
kufanya lolote.
Hata Prisons ambao ni wakongwe na ligi kuu
wanaweza kuwazuia Yanga leo, lakini itawabidi wafanye kazi ya ziada.
Hata historia inawahukumu wanapocheza na Yanga
uwanja wa Taifa. Mechi mbili za mwisho walifungwa 3-1 na 5-0.
Licha ya kufungwa, hawakucheza kabisa mpira.
Lakini sahizi wamejijenga upya chini ya kocha David Mwamwaja. Wana morali
kubwa, wana wachezaji mchanganyiko, nadhani wanaweza kutoa changamoto.
Yanga wanaweza kuifunga Prisons, lakini ikitokea sare au kufungwa wasishangae. Ni matokeo yanayoweza kutokea kabisa.