Published On:Ijumaa, 26 Septemba 2014
Posted by Hisia
KWIZERA, KIONGERA WAPATIWA VIBALI VYA KUPIGA KAZI SIMBA SC, CHA OKWI CHADUNDA…SABABU HAIJULIKANI
Pierre Kwizera atapiga kazi kama kawaida Simba SC baada ya kupatiwa kibali.
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
IDARA
ya Uhamiaji Tanzania imetoa vibali vya kufanyia kazi kwa wachezaji
wawili wa Simba SC, Mrundi Pierre Kwizera na Mkenya Paul Kiongera pamoja
na kocha wao, Patrick Phiri, lakini haijatoa kibali cha mshambuliaji
Mganda Emmanuel Okwi.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN
ZUBEIRY jioni hii kwamba wamefanikiwa kupata vibali vya wachezaji hao na
kocha Phiri, lakini pamoja na kupeleka pia maombi kwa ajili ya kibali
cha Okwi, hakijatoka.
“Bado
hatujajua sababu za kutotoka kwa kibali cha Okwi, lakini tunaendelea
kufuatilia ili tujue, kwa sababu huyu ni mchezaji wetu halali, ambaye
tulikamilisha taratibu za kumsajili baada ya mkataba wake na klabu yake
ya awali, Yanga SC kuvunjika,”amesema Poppe.
Mapema
jana, Idara ya Uhamiaji iliwazuia wanne hao kufanya kazi Simba SC hadi
hapo watakapopatiwa vibali- lakini sasa wanaweza kuendelea na kazi,
kasoro Okwi ambaye kibali chake kimekwama.
Simba
SC inashuka dimbani Jumamosi hii kumenyana na Polisi Morogoro katika
mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na maana yake iko hatarini kumkosa Okwi.
Okwi
anaweza kukosekana katika wakati ambao Simba SC inamkosa mshambuliaji
mwingine, Kiongera ambaye ni majeruhi anayetakiwa kuwa nje kwa wiki
sita.
Simba
SC pia itawakosa kipa Ivo Mapunda, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na
winga Haroun Chanongo ambao wote ni majeruhi, lakini habari njema tu ni
kwamba kiungo ‘mchapakazi’ Jonas Mkude yuko tayari kuanza kazi Jumamosi.
Mapunda
ni majeruhi wa muda mrefu kama Kiongera, ambaye anatakiwa kuwa nje kwa
wiki nane, wakati Issa na Chanongo wiki ijayo wanaweza kurudi kazini.
Haijulikani ‘zengwe’ la Okwi litachukua muda gani kumalizika kabla ya mchezaji huyo kurejea uwanjani.
Simba
SC ilianza Ligi Kuu kwa sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga Uwanja wa
Taifa, Jumapili iliyopita licha ya kuongoza kwa 2-0 hadi mapumziko-
maana yake itahitaji ushindi Jumamosi ili kujiweka mguu sawa katika mbio
za kuwania ubingwa.