Published On:Ijumaa, 26 Septemba 2014
Posted by Hisia
MASHABIKI 250 NDANDA FC KUTINGA MOROGORO
Mashabiki
wapatao 250 wa Ndanda fc ya Mkoani Mtwara wanaondoka kesho saa
mbili usiku kuelekea mkoani Morogoro, kwenda kuiunga mkono timu yao itakayoshuka
dimbani jumamosi kumenyana na wenyeji wao Mtibwa Sugar katika uwanja wa
jamhuri.
Mashabiki
hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kundi hilo Salumu Mabomba wamehamasika na kuwa
na imani na timu yao baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa
kwanza wa ufunguzi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara dhidi ya Stand United
mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mashabaki
hao ambao wamepania kuwaziba midomo wakata miwa baada kushinda 2-0 katika
mchezo wao wa awali dhidi ya Yanga uwanja wa Jamhuri na wameona ni lazima
kuwapa morari wachezeji ili waweze kucheza kwa bidii na kuondoka na pointi
tatu.
Kila inapofika mwishoni mwa wiki, mashabiki wa
Ndanda fc iliyopanda daraja msimu huu wamekuwa wakikutana kupanga mikakati na
kila mwanachama hutoa mchango wa sh 3000 kwa ajili ya nauli ya kusafiri na timu hiyo
kila inapokwenda kucheza nje ya uwanja wao wa nyumbani wa Nangwanda.
Akizungumza na mtandao
huu mwenyekiti wa kundi hilo maarufu
kama Ndanda fc kwa roho safi, Salumu
Mabomba, amesema maandalizi ya kuelekea mkoani Morogoro yamekamilika na watu
250 tayari wana uhakika wa kwenda.
“Tunaondoka saa mbili usiku kesho ijumaa
kuelekea Morogoro kwenda kuipa nguvu timu yetu ya Ndanda na tunataka kuwaonesha
watanzania kwamba hatuna masihara katika hili na tunaipenda timu yetu na hatuwezi
kuiangusha hata siku moja. Mtibwa wajiandae
na kichapo tu na Vijana wana hamasa kubwa , magari madogo sita yatabeba
watu 50, mabasi makubwa manne yatabeba watu 200,” alisema Mabomba.
Alisema kuwa baadhi ya wadau wamejitokeza na kuwapatia nguvu kwa swala la usafiri kwa kuwapunguzia bei, hivyo wamewashukuru waendelee kuwa na moyo kama huo na wale ambao wako tayari kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri wanaombwa kujitokeza hata kwa kitu chochote kwa mashabiki hao ambao wameamua kujitoa kwa ajili ya kuiunga mkono timu hiyo.