Published On:Ijumaa, 19 Septemba 2014
Posted by Hisia
Baadhi ya vigogo Simba, Yanga watajwa Kuihujumu Taifa Stars
Kikosi cha Taifa stars.
Na Mwandishi wetu
SIRI za kushindwa kwa timu ya soka ya taifa kufuzu katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).
Siri
hiyo ya kukwama kwa timu ya taifa kwenye michuano ya (AFCON), inadaiwa
kutokana na hujuma zilizofanywa na kundi la watu wachache kwa lengo la
kumwonesha Rais wa TFF, Jamal Malinzi hawezi kuongoza shirikisho hilo
na kuipa mafanikio Stars.
Wahujumu hao wa soka nchini, wanadaiwa kutoka katika vilabu vikubwa vya soka nchini ambao kwa sasa majina yao yamehifadhiwa.
Uchunguzi
uliofanywa tangu timu ya soka ya taifa ilipotolewa kwenye michuano hiyo
na timu ya soka ya Msumbiji, unaonyesha kuwa hilo limeapa kufanya
hujuma dhidi ya timu ya taifa ili kumkomoa Malinzi kwa sababu ya chuki
na minyukano ya makundi yaliyoibuka wakati wa uchaguzi wa Rais wa TFF.
Habari
kutoka ndani ya TFF zinasema kuwa katika mechi mbili na timu ya soka ya
taifa ya Msumbuji, waasi hao waliwatumia baadhi ya wachezaji wa stars
kucheza chini ya kiwango, wengine kucheza rafu za makusudi na kumwaga
fedha kwa mmoja wa waamuzi na matokeo ya mchezo huo yaliishia kwa sare
ya bao 1-1.
Katika
mchezo wa marudiano uliofanyika wiki mbili baadaye mjini Maputo, Stars
ilitolewa kwa kufungwa bao 2-1, huku ikinyimwa penalti na kukataliwa bao
lingine katika mazingira ya kutatanisha.
“Katika
mechi zote mbili, kundi hilo liliwatumia baadhi ya wachezaji kucheza
chini ya kiwango na kumhonga mmoja wa waamuzi fedha. Fedha hizo
zilikabidhiwa kwa mchezaji mmoja wan je anayecheza soka la kulipwa
katika moja ya vilabu vikubwa nchini ambaye naye alimkabidhi mwamuzi
huyo aliyeiua Stars,” alisema mtoa habari wetu.
Uchunguzi
umebaini kuwa tayari Serikali imeagiza kuunda tume ya kuchunguza kashfa
hiyo na kuapa kuwachukua hatua dhidi ya watakaobainika kuhusika na uasi
huo dhidi ya timu ya taifa.
Malinzi
aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, amekutana na wakati
mgumu ndani ya Shirikisho hilo, licha ya kufanya maandalizi makubwa kwa
timu hiyo, kuiwezesha kushiriki michuano ya AFCON.
Katika
maandalizi ya mwaka huu, stars ilipewa maandalizi makubwa chini ya
udhamini mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake
cha Kilimanjaro.
Licha
ya udhamini huo, pia Serikali imekuwa karibu na TFF kuhakikisha timu ya
soka inafanya vyema na kuondokana na aibu ya kugeuzwa kuwa kichwa cha
Mwendawazimu.
Stars
mwaka huu ilifanya maandalizi makubwa chini ya kocha wake Mart Nooij
kwa kuweka kambi takribani mwezi mzima nchini Botoswana, na pia Tukuyu
mkoani Mbeya kwa lengo la kuhakikisha inashiriki AFCON mwakani nchini
Morocco.
“Hii
hali inasikitisha sana. Kama mtu ana bifu na Malinzi, hamfanyie yeye
lakini sio kuihujumu timu ya taifa. Kwa taarifa yako hao watu wataanikwa
muda si mrefu maana wanajulikana,” alisema mtoa habari wetu.
Alipoulizwa
juu ya kuwapo kwa hujuma hizo, Rais wa TFF Malinzi, hakukubali wala
kukataa na badala yake alisema kama kweli kuna watu wa aina hiyo, taifa
litakuwa limefika mahali pabaya.
“Mimi
katika hilo, sina cha kusema, lakini kama kuna ukweli ndani yake,
nitasikitika sana, maana hii timu siyo yangu mimi ni timu ya
Taifa,”alisema Malinzi.