Published On:Jumapili, 21 Septemba 2014
Posted by Hisia
BAADA YA KUCHABANGWA 2-0 NA WAKATA MIWA, MARCIO MAXIMO ATOA KAULI HII HAPA.
YANGA SC imeanza vibaya ligi kuu soka Tanzania
bara msimu wa 2014/2015 baada ya jana kukubali kipigo cha 2-0 katika mechi ya ufunguzi
iliyopigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar.
Ikicheza mbele ya mashabiki waliofurika kutoka Dar
es salaam, Morogoro na mikoa ya jirani, Yanga ilionesha kandanda safi na kupata
nafasi nyingi za kufunga, lakini washambuliaji wake walichemsha kuzibadili kuwa
magoli.
Yanga walicheza mpira mwingi zaidi kipindi cha
pili, wakifika golini kwa Mtibwa Sugar, lakini walijikuta wakifungwa magoli
mawili kwa staili ya mipira mirefu.
Mussa Hassan Mgosi katika dakika ya 15 kipindi cha
kwanza aliwainua mashabiki wa Mtibwa
akifunga bao la kuongoza kufuatia mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na
Kelvin Yondani kushindwa kuosha mpira mrefu uliopigwa langoni mwao.
Yanga waliongoza kumiliki mpira kipindi cha pili,
waliikalia barabara Mtibwa na kukaa langoni kwao kwa muda mrefu, huku Mrisho
Ngassa na Saimon Msuva wakitumia kasi yao kutokea pembeni na kuwahenyesha
mabeki wa timu pinzani.
Wakiwa na matumaini makubwa ya kusawazisha na
kuongeza bao la ushindi, Dakika ya 83, Ame Ali alipata mpira mrefu na kusumbuana na
Cannavaro akiwa na mwenzake Yondani, akatishia akapiga mpira wa juu
ambapo kipa Dida alipaa juu na kujaribu kuokoa, lakini ukazama nyavuni na
kuiandikia Mtibwa bao la pili.
Goli hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga
ambapo kwa muda mrefu timu yao ilikuwa ikishambulia na mpira ulipopigwa
hawakuwa tayari kukuabiliana na shambulizi hilo la kushitukiza.
Baada ya mechi hiyo, watu wengi walitamani kusikia
nini atasema kocha mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo.
Maximo alisema : “Tulicheza mpira na tukafungwa,
lakini ligi ndio inaanza. Ninachopenda kusema ni kwamba sio vizuri
kupoteza matumaini kwasababu mechi ijayo
tutaweza kuimarika na kushinda”
“Tulipoteza nafasi nyingi, mechi ilikuwa ngumu.
Walitumia nafasi zao, sisi hatukutumia nafasi zetu, ni rahisi tu, mpira wa
miguu uko hivyo. Ukipoteza nafasi unahatarisha vitu vingi”
“Kitu cha msingi ni kwamba , kamwe timu haitakata tamaa , huo ndio mpira, wakati fulani siku
inakuwa nzuri na siku nyingine inakuwa mbaya”.
Yanga watacheza mechi ya raundi ya pili septemba 28 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Tanzania Prisons iliyoshinda jana mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shootings uwanja wa mabatini, Mlandizi, Mkoani Pwani.