Published On:Jumapili, 21 Septemba 2014
Posted by Hisia
JE, PAUL KIONGERA ATAZIDI KUMZIMA KIAINA AMISSI TAMBWE LEO?
PAUL Kiongera leo jioni anatarajia kuiongoza Simba
dhidi ya Coastal Union katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu soka Tanzania bara
itakayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Kiongera anayeonekana kufunika jina la mfungaji
nyota wa Simba msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe, anatazamwa kwa jicho la
tatu kutokana na kiwango chake alichoonesha kwenye mechi ya kimataifa ya
kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, septemba 6 mwaka huu na nyinginezo.
Mbali na kufunga mabao mawili katika ushindi wa
3-0, Kiongera alionesha soka safi na kukonga nyoyo za mashabiki wa Simba
waliofurika kwa wingi uwanjani.
Simba walionekana kubadilika katika mechi hiyo
wakicheza soka la chinichini, pasi za uhakika na kupanga mashambulizi mazuri
kutokea sehemu ya kiungo.
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Seleman, Shaaban
Kisiga, Okwi, Kiongera walionekana kuwa katika ubora wa juu.
Katika mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki,
Simba walifungwa bao 1-0 na URA ya Uganda na kutoka suluhu ya bila kufungana na
Ndanda fc katika mechi ya mwisho ya kujipima ubavu.
Baada ya mechi hiyo, Simba wamekaa takribani wiki
moja visiwani Zanzibar na walirejea jana Dar es salaam tayari kwa mechi ya leo.
Haifahamiki ni kwa kiasi gani kocha Patrick Phiri
amefuta makosa yaliyojitokeza katika mechi za mwisho za kirafiki kwasababu
hajacheza mechi nyingine, lakini katika mazoezi ya Zanzibar, Simba walionekana
kuwa imara.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa Simba walizidi
kumuonesha Phiri kuwa wanajua wanachokifanya ingawa msimu uliopita waliangushwa
na kocha aliyetimuliwa Zdravko Logarusic.
Phiri amekuwa akiwafundisha vijana wake jinsi ya
kujilinda, kupiga pasi za uhakika, kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi.
Utamaduni wa soka la Tanzania hususani Simba sc ni
mpira wa pasi ‘passing football’ na mashabiki wengi wanapenda hivyo.
Katika mechi dhidi ya Gor Mahia walionesha ladha
ya mpira huo uliopotea kwa muda mrefu, ingawa katika mechi ya URA hawakucheza
katika kiwango chao.
Leo Simba wanakutana na Coastal Union wakiwa na
sura mpya kikosini baada ya kufanya usajili mzuri.
Wachezaji kama Tshabalala, Shaaban Kisiga, Piere
Kwizera, Kiongera, Emmanuel Okwi, Abdi Banda na wengineo ambao hawakuwepo msimu
uliopita wanaweza kuanza.
Coastal Union imekuwa katika mabadiliko makubwa
kuanzia uongozi, wachezaji, na wadhamini.
Msimu uliopita walikuwa wanadhaminiwa na Binslum,
lakini walivunja ‘ndoa’ hiyo na sasa wanaendelea na maisha mengine chini ya
wadhamini wengine.
Waliweka kambi ya mwezi mmoja kisiwani Pemba na
wamecheza mechi nyingi za kirafiki kwa malengo ya kujiimarisha.
Matundo ya maandalizi hayo yanatarajia kuonekana
katika mechi ya leo wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Simba 1-0 katika mechi ya
mzunguko wa pili msimu uliopita.
Mashabiki wa Simba wamekuwa na imani na kikosi
chao kwa sasa, na kwa vile Mtani wao alifungwa jana 2-0 na Mtibwa Sugar, basi
itakuwa furaha kubwa kama wataanza kwa ushindi.
Haitakuwa mechi rahisi hata kidogo kwa Simba licha
ya kuwa uwanja wa nyumbani. Coastal Union wana historia ya kufanya vizuri dhidi
ya Simba hususani wakiwa uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani.
Hii itakuwa mechi ngumu sana, lakini kutokana na
namna Simba ilivyojengwa vizuri na Phiri, nathubutu kutoa asilimia 60 za
ushindi dhidi ya 40 za Coastal Union.
Yawezekana matokeo yakawa tofauti kama ilivyokuwa kwa Yanga jana, lakini nawapa nafasi kubwa zaidi Simba kushinda, ingawa mechi itakuwa ngumu na tunaweza kushuhudia lolote lile.