Published On:Jumatano, 10 Septemba 2014
Posted by Hisia
KUMSHINDA EMMANUEL OKWI FIFA SIO RAHISI KWA YANGA, LABDA INAWAUMA HANS POPPE KUPATA POINTI 3 MUHIMU
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange 'Kaburu' (kushoto) na Emmanuel Okwi (kulia) wanakumbushia zile 5-0 ?
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
EMMANUEL Okwi kwasasa ndiye mchezaji anayetamkwa zaidi
midomoni mwa mashabiki, wadau, viongozi, wanasheria na kila mtu anayependa
mchezo wa soka nchini.
Okwi ni miongoni wa Waganda wachache waliopata
umaarufu nchini Tanzania kwa sababu kubwa mbili.
Mosi; Aina ya uchezaji wake. Huyu ni Mganda
anayeonesha kiwango kikubwa kwa wachezaji wa kigeni nchini Tanzania. Akiwa
Simba miaka ya nyuma alikuwa moto wa kuotea mbali (kumbuka kipigo cha 5-0
walichopata Yanga), lakini hakufanya vile vile alipotua Yanga mwezi desemba
mwaka jana.
Pili; umaarufu wa Okwi unatokana na namna
anavyowapa shida viongozi wa Yanga na Simba. Akiwa Msimbazi, alikuwa na tatizo
la kuchelewa kurudi kambini pale anapopewa ruhusa ya kwenda Uganda. Hili ni
tatizo aliloliendeleza hata alipokwenda Etoile Du Sahel ya Tunisia akitokea
Simba na aliporudi Yanga akitokea Sports Club Villa ya Uganda aliendelea na
kamchezo haka.
Licha ya kuwa msumbufu kwenye baadhi ya mambo hasa
nidhamu ya kuheshimu mipango ya kambi ya timu, Okwi ni mchezaji hatari uwanjani
na pengine ndio maana kila mtu anapenda kuwa naye kwenye kikosi chake.
Simba licha ya kuwahi kusumbuliwa mara kadhaa na
Okwi, hawajaona haja ya kutomsajili kwasababu wanaamini atawasaidia wakati huu
wanajenga kikosi chao.
Okwi, Amiss Tambwe, Paul Kiongera, Ramadhan
Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo, Kisiga, Uhuru Seleman wanatazamiwa kuifanya
safu ya ushambuliaji ya Simba kuwa na makali msimu ujao.
Kwasasa Okwi anazungumzwa mno na sababu kubwa sio
kusajiliwa Simba, bali ni mgogoro wa kimkataba baina yake na klabu yake ya
zamani ya Yanga.
Safari hii Simba hawana tatizo na Yanga katika
usajili wa Okwi, ila mchezaji anaumana kisheria na Yanga chini ya mwenyekiti
aliyetangaza kuifanyia kitu kibaya Simba kwa madai kuwa imemsajili mchezaji
mwenye mkataba, Yusuf Manji.
Mtu hatari Paul Kiongera (kushoto jezi nyekundu) ataungana na Okwi safu ya Ushambuliaji Simba sc
Yanga walimshitaki Okwi kwa kitendo cha kusaini
mkataba na klabu nyingine wakati ana mktaba wa miaka miwili na nusu na
Wanajangwani hao, lakini Septemba 7 mwaka huu kamati ya Sheria na Hadhi za
wachezaji ya Shirikisho la soka la Tanzania, TFF, ilikuja na majibu Tofauti.
Kamati hiyo chini ya Mwanasheria mashuhuri na
mwenye msimamo, Richard Sinamtwa iliupitia mkataba wa Okwi na Yanga, ikatafsiri
kanuni na kugundua kuwa Yanga walishindwa kutekeleza kipengele cha 8 cha
mkataba huo ambacho kinahusisha mambo kadhaa, lakini ikiwemo malipo ya ada ya
usajili wake.
Kutokana na kukiukwa kwa kipengele hicho cha
kimkataba, kamati ilibaini kuwa mkataba wa Yanga na Okwi ulishavunjika siku
nyingi na walimtangaza kuwa mchezaji huru.
Kabla ya hapo Yusuf Manji aliwahi kutamba kuwa
Okwi hatacheza Simba kwasababu ni mchezaji wao. Alitangaza kumshitaki Okwi na
alisema lazima ailipe Yanga fidia.
Lakini kumbe kuna mapungufu mengi kwenye mkataba
na baada ya kupitiwa imeonekana Yanga ndio walivunja mkataba, hivyo wanatakiwa
kumlipa Okwi kwasababu ya Usumbufu huo.
Lakini kama kawaida, Septemba 8 mwaka huu, uongozi
wa Yanga ulipinga maamuzi ya kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya
kumtangaza mchezaji wake, Emmanuel Okwi kuwa huru.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya
Yanga, Sam Mapande aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawajaridhishwa na
maamuzi hayo ambayo yanakinzana na shitaka zima la mchezaji huyo.
Mwenyekiti wa kamati ya sheria na utawala bora wa Yanga, Wakili Sam Mapande (kulia)
Mapande alisema kuwa kamati ya TFF imeamua
sakata la Okwi kinyume na malalamiko yao kwani hakukuwa na lalamiko la mchezaji
huyo wa Uganda kuhusiana na malipo ya fedha zake za usajili.
Alisema kuwa cha kushangaza, kamati hiyo ya
TFF iliamua kusikiliza kesi ambayo haikuwa mbele yao na kutoa maamuzi ambayo
hata wao wameshangazwa nayo.
“Kwanza kesi yenyewe ilikuwa haijamalizika,
walituambia tuwasilishe vielelezo kuhusiana na kitendo cha mchezaji huyo
kufanya mazungumzo na klabu ya Misri, lakini cha kushangaza maamuzi yametolewa,
hili limetushangaza sana,” alisema Mapande.
Alisema kuwa mazingira yalikuwa yameandaliwa
kuibeba Simba na Okwi kwani hata malalamiko yao kwa Simba hayakusikilizwa.
“Malalamiko yetu yalikuwa wazi kabisa, yapo
kimaandishi, hatukuwahi kulalamikiwa, suala la fedha za usajili la Okwi
limetoka wapi, kama lilikuwepo, mbona hatujajulishwa kimaandishi kama utaratibu
ulivyo,” alisema.
Pia alipinga kitendo cha kamati hiyo
kumruhusu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Zacharia Hans Pope ambaye pia ni
mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba kuwemo katika kikao hicho kinyume na
taratibu za Fifa kupitia kifungu namba 19 kinachoeleza mgongano wa kimaslah.
Dkt. Damas Daniel Ndumbaro
Jana wakili aliyemsimamia Okwi, mwanasheria
mashuhuri nchini na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas Ndumbaro katika
taarifa yake kwa Umma alisema mbele ya Kamati, Yanga
walileta hoja kuwa: Hans Pope ana mgongano wa maslahi kwa kuwa amemsajili Okwi
Simba na yeye ni mjumbe wa Kamati hii. Okwi amekataa kuongeza au kupunguza
mkataba kama ilivyopendekezwa na Yanga; Okwi ameleta madai yasiyo na msingi ya
kutaka apewe nyumba ya kuishi; hajacheza mechi 6 hivyo kuikosesha Yanga
ubingwa. Okwi amefanya makubaliano na Klabu ya Wadi Geldi ya Misri wakati ana
mkataba na Yanga. Hivyo basi Yanga waliitaka Kamati itamke kuwa mkataba kati
yao na Okwi umesitishwa, imfungie Okwi kucheza mpira Tanzania Maisha na ailipe
Yanga dola za kimarekani laki mbili.
Ndumbaro akimwakilisha
Okwi, alitoa hoja kuwa: Mteja wao amekubali ombi la Yanga la kuvunja mkataba
ambalo limo katika barua zake nne; Yanga ndio wamevunja mkataba kwa kushindwa
kulipa signing fee US$ 50,000; Mishahara ya miezi mitano US$ 15,000 na kodi ya
nyumba US$ 2,800. Madai hayo ni kwa mujibu wa mkataba.
Baada ya Maswali toka kwa
Kamati kwa pande zote mbili, Yanga waliomba kufuta barua zao, ombi ambalo
lilitupiliwa mbali na kamati.
Ndumbaro alisema kamati,
hatimaye ilifanya maamuzi ya kihistoria katika kulinda haki za kimkataba za
wachezaji kama ambayo imeelezwa hapo juu.Kwa mtu yoyote mwenye akili timamu,
anapaswa kuipongeza kwa dhati kamati kwa maamuzi ambayo wanajenga mpira wa nchi
hii. Vilabu vinapaswa kufahamu kuwa haki za mchezaji lazima ziheshimiwe.
Mwanasheria huyo
aliongeza kuwa hoja za Yanga kuwa hakukuwa na madai ya fedha sio sahihi
kwasababu Majibu toka kwa Okwi na mabishano ya maneno mbele ya kamati hiyo
ilijadili kwa kina madai ya fedha ya Okwi na hata Yanga walikiri kutolipa madai
hayo. Hivyo basi si sahihi kusema kuwa eti suala la madai ya fedha
halikujadiliwa. (ona kiambatisho MNA1)
Msingi wa malalamiko ya
Yanga ni barua ya tarehe 27 Juni 2014, ambayo hakuna sehemu ambayo inatamka
suala la Simba. Kama kuna kesi dhidi ya Simba, wasubiri wakati wa kupitia
pingamizi za usajili lakini suala ambalo Yanga walilalamikia ni kusitisha
mkataba na Okwi na madai ya fidia.
Kamati ya Sheria na
Mwenyekiti wake hawana mamlaka ya kujadili uteuzi au uwepo wa Hans Pope kwenye
kikao hicho. Mamlaka ya Uteuzi ndio, kwa mujibu wa katiba ya TFF, yenye uwezo
wa kutoa uamuzi kuhusu suala hilo.
Okwi enzi hizo akisajiliwa Yanga sc
MGOGORO KATI YA YANGA NA
OKWI KWA MUJIBU WA TAARIFA YA NDUMBARO
Mkataba wa Yanga na Okwi,
ambao ulisainiwa tarehe 12 Disemba 2014 umekuwa na mapungufu yafuatayo:
1. Mkataba
huo umempa majukumu mchezaji kufuatilia ITC na suala zima la yeye kupata vibali
vya kucheza. Hii ni kinyume na Kanuni za FIFA ambao zinatamka bayana kuwa
jukumu la kufuatilia ITC ni la wanachama wa FA, lakini Yanga walimtwisha Okwi
zigo hilo. Okwi alitekeleza jukumu hilo.
Kamati ililiona hilo na
kusema wazi kuwa hilo sio sahihi. Ni vema wachezaji wajue kuwa hilo sio jukumu
lao.
2. Pili
Yanga, kwa mujibu wa mkataba, walikuwa na haki ya kumkata mchezaji theluthi
moja ya mshahara wake wa mwezi endapo atakosa mechi tatu au zaidi. Yanga
walimkata Okwi Mishahara ya miezi mitano, kinyume na matakwa ya mkataba na
pasipo maelelzo yoyote.
3. Yanga
na Okwi walikubaliana kuwa mchezaji atalipwa ada ya kusaini mkataba (signing on
– fee) ya US$ 100,000, kwa Awamu mbili. Awamu ya kwanza wakati wa kusaini
mkataba na awamu ya pili tarehe 27 Januari 2014. Mpaka hivi sasa, Yanga
wamelipa US$ 50,000 tu na bado kuna deni la US$ 50,000. Huu ni uvunjaji wa
mkataba wa wazi kabisa.
4. Kipindi
chote mchezaji akiwa na klabu ya Yanga, hajapewa nyumba kama ambayo
walikubaliana. Huu ni ukiukwaji mwingine wa mkataba.
Baada ya Okwi kuanza
kudai haki zake tajwa hapo juu, Yanga waliamua kutomlipa mteja wetu mishahara
ya miezi mitano kinyume na matakwa ya mkataba kati yao.
Furaha iko wapi?: Okwi alipokuwa akiwapungia mkono mashabiki wa Yanga baada ya kutua nchini desemba mwaka jana
MPANGO WA SIRI WA YANGA KWA MUJIBU WA NDUMBARO
Yanga walikuwa na mpango wa siri wa kuvunja
mkataba na Emmanuel Okwi ili wamkomoe mteja wao, ashindwe kucheza mpira,
kiwango chake kiporomoke na itumike kama onyo kwa wachezaji wengine ambao wanadai
haki zao. Mpango huu ulitekelezw kama ifuatavyo:
a. Tarehe
27 Juni 2014, Yanga waliandika barua kwenda TFF, ikiitaka TFF, pamoja mambo
mengine, itambue kuwa mkataba kati yao na Okwi umefutwa. Barua hiyo haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
b. Tarehe 25
Julai 2014, Yanga waliandika barua ya pili kukumbushia barua yao ya tarehe 27
Juni 2014. Barua hiyo ya pili haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande
wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
c. Tarehe
20 Agosti 2014 Yanga waliandika barua nyingine tena wakikumbushia hoja zao
tajwa hapo juu. Kwa mara ya tatu, barua hiyo haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye
ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
d. Yanga
waliandika barua nyingine ya nne tarehe 25 Agosti 2014 ikiwa na hoja zile zile
za kusitisha mkataba na mteja wetu. Kwa mara ya nne barua hiyo haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
Baada ya TFF kupanga tarehe ya kikao cha Kamati ya
Sheria na hadhi ya wachezaji na kutoa barua ya wito tarehe 27 Agosti 2014 ndipo
kwa mara ya kwanza mchezaji Emmanuel Okwi akafahamu kuwa Yanga wameomba kuvunja
mkataba wake.
Tarehe 27 Agosti 2014, Emmanuel Okwi aliiandikia
Yanga KUKUBALI ombi lao la kuvunja mkataba.
Okwi aliwashinda Etoile Du Sahel katika kesi iliyosikilizwa FIFA
Kimsingi ukiangalia maelezo ya pande zote, dhahiri
Yanga wapo katika wakati mgumu kwasababu kuna mapungufu mengi katika mkataba
baina yake na Okwi.
Kama nilivyosema juzi, Okwi ni mchezaji mahiri
uwanjani, lakini amekuwa makini sana katika masuala ya kisheria hasusani kwa
mambo yanayogusa maisha yake ya soka.
Aliibwaga Etoile Du Sahel iliyoenda kwa mbwembwe
FIFA kumshitaki kuwa ni mchezaji wake baada ya nyota huyo kusema hana mkataba
na klabu hiyo.
Ni kweli Okwi alikuwa ni mchezaji wa klabu hiyo,
lakini Etoile walijitia kitanzi baada ya kutomlipa mshahara wake kwa miezi
mitatu mfululizo wakidai ni adhabu.
Okwi aliruhusiwa na klabu hiyo kwenda kuitumikia
Uganda, lakini alichelewa kurudi Tunisia na ndipo klabu yake ikatangaza kumpa
adhabu ya kutomlipa mshahara kwa miezi mitatu na kushushwa mpaka timu B.
Lakini Mganda huyu alisimama kidete na kuwagomea
na ndipo walipomshitaki FIFA. Alitafsiri kipengele kimoja cha mkataba kuhusu
mshahara ambapo kilieleza kuwa kama mchezaji hatalipwa mshahara kwa miezi
mitatu, mkataba utavunjika.
FIFA waliliona hilo wakampa ushindi Okwi na kuwa
mchezaji huru wakati huo alikuwa ana mkataba wa muda na Villa ya Uganda ambao baadaye
walimuuza Okwi katika klabu ya Yanga.
Ukifuatilia kwa makini, Okwi aliwashinda Du Sahel
kwa kipengele cha kukwepa matakwa ya kimkataba na ndivyo ilivyo kwa Yanga.
Yanga wanatamba kuwa na mkataba na Okwi, kumbe
kuna vipengele hawajatekeleza kwa mujibu wa makubaliano.
Mkataba ni kama ndoa. Lazima uheshimiwe kwa pande
zote mbili.
Unapotaka kumsajili mchezaji unamuita na kukaa
naye mezani ( Kama ni mchezaji huru), lakini kama ana mkataba na klabu
nyingine, lazima uwasiliane na timu yake.
Mwenyekiti wa Yanga sc, Yusuf Manji
Hali kadhalika unapotaka kuvunja mkataba hutakiwa
kufanya siri bila kumjulisha mchezaji. Kwasababu unahusisha pande mbili, lazima
mchezai apewe taarifa kwa maandishi na yeye ajibu kwa maandishi, lakini Yanga hawakufanya
hivyo kwa Okwi.
Kamati ya usajili ya Simba chini ya Zacharia Hans
Poppe ilizungumza na Okwi na sio Yanga kwasababu ilijiridhisha kuwa ni mchezaji
huru na kweli wamefanikiwa.
Nadhani Hans Poppe alishauriwa vizuri na
wanasheria wake na yeye hakuwa na shaka juu ya usajili huo na ndio maana kila
akiongea anajiamini kuwa yuko sahihi.
Lakini ushindi huu wa Hans Poppe unawaumiza kichwa
vigogo wa Yanga ambao wanasema wanakwenda FIFA kukata rufaa.
Kuna jambo la msingi Manji lazima ashauriwe
vizuri. Kweli Rufaa ni haki ya msingi ya kisheria na pale unapoona hujatendewa
haki, unaruhusiwa kusonga mbele kwa kukata rufaa.
Lakini kuna mambo mawili hutokea, Rufaa yako kushinda
au kutupiliwa mbali.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, 'Big Boss', Zacharia Hans Poppe
Ukishinda rufaa maana yake maamuzi ya awali
yanafutwa, ukishindwa lazima ufuate maamuzi ya awali.
Maana yake kama rufaa ya Yanga itakubaliwa na
FIFA, itakuwa hasara kwa Okwi na Simba kwani watalazimika kulipa fidia kubwa
kwa makosa wanayodaiwa kufanya, kwa mujibu wa Yanga.
Lakini kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji ya TFF
haijaona kosa la Okwi wala Simba, lakini Yanga bado wanaamini kuna makosa yapo
na hawajatendewa haki.
Lakini kama FIFA watampa ushindi Okwi, basi
litakuwa pigo lingine kwa Yanga. Na hapo watatakiwa kumlipa mchezaji bure
kabisa na hawatachomoka mbele ya FIFA.
Kwahiyo Manji lazima ajue mambo haya mawili. Ni
muhimu kukaa chini na washauri wake, kupitia vizuri mkataba na sheria, ndipo
waende FIFA. Kama wataingia kichwa kichwa kwa kupamba leongo la kupambaa na
Hans Poppe wanaweza kufungwa bao la tobo.
Mambo ya kisheria ni yale yale, usidhani kama
kamati ya sheria na Hadhi ya Wachezaji imetumia sheria za Tanzania. Hizo ni
sheria za FIFA.
Hata kama Yanga watakwenda kule, lazima FIFA
watahitaji muhstari wa maamuzi ya kamati ya TFF na kuyapitia, baada ya hapo
watasikiliza pande zote mbili, Okwi na Yanga na hatimaye kutoa maamuzi.
Kama Yanga wameshindwa kutekeleza matakwa ya
kimkataba uliopo katika maandishi na umesainiwa na viongozi wa juu, basi FIFA
watatoa maamuzi yanayofanana na ya kamati ya TFF.
Kuna wakati sheria ni kama hesabu, 1 + 1 = 2, na
jibu haliwezi kuwa 3. Kama Yanga wamekosea kwa mujibu wa sheria, haitawasaidia
kukata rufaa, labda busara itumike kama ilivyozoeleka.
Ninachokiona hapa, Yanga hawataki kukubali. Na hii
pengine inatokana na Ufalme wa Yusuf Manji. Tayari alishatoa tamko, sasa inakuwa
ngumu kurudi na kulifuta au kuomba radhi.
Sio utamaduni wa timu za Simba na Yanga kutoswa
TFF, na ndio maana maamuzi kama haya yanawaumiza Yanga. Kwa bahati mbaya
yanawahusishwa watani zao wa jadi ambao nao walilia suala la Mbuyu Twite.
Kwa utamaduni wa viongozi wa Tanzani, sio wepesi
kukubali kukosea kwasababu wanaona kama ni kujidharilisha tu. Lakini kwa Manji
inatakiwa apitie vizuri sheria au ashauriwe vizuri kabla ya safari ya FIFA.
Itamuumiza zaidi kama atafungwa goli lingine kule
FIFA. Kama wameona wamekosea, wangetulia tu na kuendelea na maisha mengine.
Okwi ni mjanja sana, ukiingia kichwa kichwa,
lazima uumbuke tu.
Lakini kuna kitu cha msingi Hans Poppe lazima
ajue. Suala la Okwi huenda likawafumbua macho wachezaji wengi wa Tanzania ambao
mikataba yao huchezewa hovyo.
Ni muhimu kuipitia mikataba hiyo pamoja na ya
wachezaji wa zamani wenye madai Simba ili kumaliza matatizo yaliyopo. Na hata
Yanga nao wajiangalie juu ya hili , kwasababau kama wachezaji wote wataibuka,
hali itakuwa tete kweli kweli.
Siku njema!