Published On:Jumatano, 10 Septemba 2014
Posted by Hisia
YANGA KUJIFICHA BAGAMOYO KUIWINDA AZAM FC, BOCCO NJE WIKI TATU
YANGA SC ina mpango wa kuweka kambi mjini Bagamoyo mkoani
Pwani kujiandaa na mechi ya ngao ya Jamii kuashiria kuzinduliwa kwa msimu mpya
wa ligi kuu soka Tanzania bara itayopigwa jumapili (septemba 14 mwaka huu) uwanja
wa Taifa Dar es salaam.
Kiingilio cha chini katika mechi hiyo inayowakutanisha
mabingwa na washindi wa pili wa msimu uliopita kitakuwa shilingi elfu 5 tu kwa
viti vya kijani na bluu.
Viti vya rangi ya chungwa ni Tsh. 10,000, VIP C na B itakuwa
20,000/=, wakati VIP A ni Tsh. 30,000 na tiketi za elekroniki zitatumika katika
mechi hiyo.
Msimu uliopita, Azam walitwaa taji wakati Yanga chini ya
kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm walishika nafasi ya pili.
Uongozi wa Yanga umeamua kumchagulia eneo la Bagamoyo kocha
Marcio Maximo ili kuwatuliza zaidi wachezaji wake.
Mara kadhaa msimu uliopita, Yanga walijichimbia Bagamoyo
kujiandaa na mechi za ligi kuu na ligi ya mabingwa barani Afrika.
Wakati huo huo, Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, Azam fc wanaendelea
kujiandaa na mechi hiyo katika uwanja wao wa kisasa wa Azam Complex, uliopo
Mbande , Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Aggrey Maris aliyeikosa mechi ya kirafiki baina ya Taifa
Stars na Burundi septemba 7 mwaka huu mjini Bujumbura kutokana na majeruhi,
amerejea katika mazoezi hayo.
Lakini taarifa mbaya ni kwamba, nahodha wa klabu hiyo, John
Bocco ‘Adebayor’ licha ya jana kufanya mazoezi katika Gym ya kisasa pale
Chamazi-Azam Complex, vipimo alivyofanyiwa na mtaalamu (Physiotherapist),
Gilbert Kigade katika Hospitali ya Msasani Peninsula vinaonesha kuwa nyota huyo
mkali wa kufumania nyavu anatakiwa kukaa nje ya uwanja wa kwa wiki tatu.
Kwa maana hiyo, Bocco anayesumbuliwa na maumivu ya misuli
ataikosa mechi ya jumapili dhidi ya Yanga na pia michezo mitatu ya ligi kuu
soka Tanzania bara inayotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.