Published On:Jumatatu, 8 Septemba 2014
Posted by Hisia
Phiri: Yanga,Azam imekula kwenu
Mshambuliaji wa Simba, Raphael Kiongera (kulia) akishangilia
na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza katika mechi ya kirafiki ya kimataifa
dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi. Simba
ilishinda 3-0. Picha na Michael Matemanga.
KOCHA Patrick Phiri ameangalia uwezo wa Emmanuel
Okwi na Paul Kiongera akawaambia Yanga na Azam akisema: “Kwa muziki huu imekula
kwenu aisee.”
Mzambia huyo anayeaminika zaidi miongoni mwa
mashabiki na wanachama wa Simba, amesisitiza kwamba kombinesheni ya mafowadi
hao ni matata sana na wana sifa ambazo zitawaziba midomo wale waliokuwa
wakiibeza Simba.
Mashabiki wa Yanga na Azam wamekuwa wakiibeza
Simba kwa madai kwamba imesajili kikosi cha kawaida ingawa kipigo cha mabao 3-0
ilichotoa kwa mabingwa wa soka wa Kenya, Gor Mahia, juzi Jumamosi
kimewafanya watikise vichwa kwa kukubali hasa makali ya Kiongera na kumzomea
Okwi.
Okwi ana utata na Yanga baada ya kusaini Simba
huku akiwa na mkataba nao jambo ambalo mpaka jana Jumapili jioni lilikuwa
likiwaumiza vichwa vigogo wa TFF ambao walikuwa na kikao cha kufanya uamuzi
kwenye hoteli ya Colesseum jijini Dar es Salaam.
Phiri ambaye si mzungumzaji sana alisema uzuri wa
Okwi na Kiongera ni kuwa wanaweza kufunga, kutafuta mipira na kupandisha
mashambulizi jambo ambalo linaongeza kasi katika safu ya ushambuliaji ya timu
hiyo.
“Ni jambo zuri kuwa na wachezaji wawili mbele
ambao wanaweza kucheza na mpira, wanajua kufunga lakini pia ni wazuri katika
kupandisha mashambulizi, hii inaongeza ufanisi wa safu ya ushambuliaji,”
alisema.
“Uwezo waliouonyesha Kiongera na Okwi kuanzia
mazoezini mpaka kwenye mechi ni wa kuvutia, wanacheza kwa kubadilika na kwa
mawasiliano mazuri kwa wakati wote, hata mabao wanayofunga yanatokana na kasi
yao.”
Phiri alipagawa zaidi baada ya kukumbuka ana
majembe yake mengine kwenye timu za Taifa ambayo yakiripoti itakuwa ni noma
zaidi.
Majembe ya Simba yaliyoko timu za Taifa ni Pierre
Kwizera na Amissi Tambwe walioko Burundi pamoja na Haroun Chanongo na Amri
Kiemba wa Taifa Stars. Bosi huyo amewaambia mashabiki wa Simba kwamba wasiwe na
presha timu yao imerudi kwenye fomu na watafanya kitu cha ajabu ambacho pengine
walikuwa hawadhaniwi kabisa wala kupewa nafasi.
Kwa upande wake Kiongera aliwatuliza mashabiki wa
Simba na kuwaambia kuwa mambo mazuri zaidi yanakuja. Juzi Jumamosi mbele ya Gor
Mahia, Kiongera aliifungia Simba mabao mawili kati ya matatu ambapo moja
lilifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’, mechi hiyo ilichezwa uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Kiongera aliliambia Mwanaspoti akisema: “Huwa
nafurahi sana ninapofunga lakini kufunga hakutatokea katika kila mechi,
inategemea na kocha amepangaje kikosi chake.
“Ila napenda kuwaambia mashabiki wa Simba kuwa
watarajie mambo mazuri kwani wachezaji wote wapo vizuri.”
Straika wa Gor Mahia Mganda, Danny Sserunkuma
alisema: “Lakini Kiongera, Okwi na Owino ni wachezaji bora katika timu ya Simba
kwa sababu nawafahamu na ni wachezaji ambao viwango vyao bado havijashuka
kabisa.
“Kurudi kwa Okwi katika timu yake ya zamani Simba
kutawasaidia sana kwani ni mtaalamu wa kutengeneza mabao na hasa wakikutana na
Kiongera Simba itapata mabao mengi zaidi.”
Chanzo: Mwanaspoti