Published On:Jumatano, 10 Septemba 2014
Posted by Hisia
PROFESSOR JAY HABANDUKI SIMBA, LIVERPOOL
MUZIKI wa ‘Hip Pop’ unazidi kuchanua nchini
Tanzania na kumekuwa na mabadiliko makubwa sana kwa miaka ya karibuni, lakini
huwezi kuuzungumzia muziki huu bila kutaja jina la Joseph Haule.
Huyu ni msanii maarufu na amedumu kwa muda mrefu katika
muziki huu wa kizazi kipya. Jina lake la kisanii linalofahamika na wengi ni Proffesor
Jay ‘Mzee wa Mitulinga’.
Tusemapo ni mkongwe, kweli ni mkongwe, kwasababu
historia yake inaonesha alianza harakati za muziki miaka 1990 akipitia makundi mbalimbali,
kabla ya kuwa msanii binafsi mwaka 2001 na kuendelea.
Akijitegemea, Professor Jay amefanya vizuri na
kushinda tuzo mbalimbali za muziki nchini.
Lengo si kuzungumzia mafanikio ya mwanamuziki huyo
kwani ana historia ndefu na ameshinda tuzo nyingi kutokana na ubora wake,
lakini leo maisha ya upande wa pili yanaangaliwa zaidi.
Ni kawaida kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya
kutumia muda wao wa ziada kufuatilia michezo mingine ndani na nje ya nchi, hususani
mpira wa miguu.
Wachezaji wa Simba sc
Kuna wasanii wengi maarufu nchini wanashabikia
timu za ndani na nje ya nchi, lakini walio wengi kwa soka la ndani ni Simba na
Yanga.
Professor Jay ni mmoja wa Wasanii wanaopenda sana
soka. Unajua anashabikia timu gani ndani na nje ya nchi? Jibu ni Simba na
Liverpool.
Katika mahojiano maalumu, Professor Jay amefurahishwa
sana na jinsi timu yake ya Simba inavyoimarika chini ya kocha Patrick Phiri na
Liverpool chini ya Brendan Rodgers.
Mkali huyo wa ‘Hip pop’ alisema ujio wa Emmanuel
Okwi kwa mara ya pili umempa faraja sana na ni ukweli Simba itakuwa hatari. Pia
alikiri kumpenda Paul Kiongera aliyesajiliwa kutoka Kenya majira ya kiangazi
mwaka huu.
Professor Jay alisema: “Okwi, kiongera nawapenda
wote. Unajua sahizi Simba inatia hamu. Napendaa ‘football’ kwa sababu inafurahisha,
jinsi inavyocheza napenda sana,”.
“Napenda sana muziki, lakini napenda sana mpira wa
miguu. Kuna wachezaji nimeanza kuwafuatilia toka zamani na natamani
wasingestaafu, mtu kama Mohamed Mwamweja, namkubali sana”.
Katika mahojiano hayo, Professor Jay aliongeza
kuwa ujio wa Okwi Simba ni jambo jema na umemrudisha nyuma hususani kipigo
walichotoa cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga mwaka 2012.
Professor alisema mechi hiyo kamwe hawezi kuisahau
kwasababu ilikuwa raha kwake ambapo Okwi alifanya kazi nzuri kuimaliza Yanga,
hivyo kurejea kwakwe anaona kipigo kingine kipo njiani.
“Okwi karudi, Simba imekuwa safi. Natamani sana
hizo mechi za ligi kuu zianze”. Aliongeza Professor Jay.
Kikosi cha Liverpool
Kuhusu Liverpool, mwamba huyo wa ‘Hip Hop’ alisema
kwa miaka mingi sana klabu hiyo haifanyi vizuri, lakini msimu uliopita
ilikaribia kutwaa ubingwa.
Aidha, alisema Liverpool iko vizuri hususani kwa
usajili wake akiwemo mshambuliaji mtukutu aliyesainishwa kutoka AC Milan, Super
Mario Balotelli.
“Liverpool tumefungwa sana, lakini sahizi tunakuja
vizuri. Balotelli (Mario) yupo pale, tutafanya vizuri. Liverpool kama kawaida
sahizi, Balotelli kaingia pale”. Professor Jay alisisitiza ujio huo wa
Balotelli
Mwisho wa yote, mtu hapotei asili yake. Ghafla
Professor Jay katika mazungumzo yake alirejea katika muziki.
Alisema kuna wimbo mkali amefanya na Diamond
Platinumz unaitwa ‘Kipi Sijasikia’.
Huu ni wimbo maarufu sana kwa siku za karibuni na
umekuwa ukipigwa sana kwenye vituo vya redio na TV, kuandikwa kwenye mitandao
na magazeti na kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Professor Jay alisema: “Nimefanya wimbo mzuri na
Diamond, umesikika sana, umepigwa sana na nilichokifanya sasa ni kutengeneza
video yake. Siku ya Jumamosi maeneo ya Makunbusho Victoria nitafanya uzinduzi
wa video hiyo. Kuna video mbili kali nazindua siku hiyo. Pia nitazindua tovuti
yangu inaitwa www.professorjay.com”.
Wakati mahojiano yanaendelea, msanii mwingine
anaangalia kwa mbali. Mwandishi analazimika kumuita ili atoe lake la moyo.
Jamaa alianza kwa kusalimia, ghafla mwandishi
kamtupia swali akisema Professor Jay ni shabiki wa Simba na Liverpool, wewe je”
Jamaa kafunguka: “ Mimi kama kawadia Simba, Man
United ingawa mmetusema sana , lakini ndio hivyo. Brazil ingawa tumefeli mwaka
huu, sio kesi, Real Madrid kama kawaida.
Bila shaka una hamu ya kumjua ni msanii gani, huyu ni msanii mwingine wa muziki wa kizazi kipya, Cpwaa.