Published On:Alhamisi, 11 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA SC KUPIGA NDEGE WAWILI KWA JIWE MOJA MWISHONI MWA WIKI
Mshambuliaji
wa Simba sc, Paul Kiongera akiruka sarakasi baada ya kuifungia Simba
bao katika mechi dhidi ya Gor Mahia jumamosi iliyopita
HAKUNA masihara kabisa!, hivyo ndivyo unavyoweza
kusema. Wekundu wa Msimbazi Simba, chini ya kocha Mzambia , Patrick Phiri, watakipiga katika mechi ya kimataifa ya
kirafiki dhidi ya URA ya Uganda uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
Perez amesema mechi hiyo ambayo ni ya mwisho ya kimataifa ya kirafiki itaanza
majira ya saa 11:00 siku ya Ijumaa ya wiki hii.
Baada ya mechi hiyo, Simba watapanda ndege
jumamosi kuelekea Mtwara ambapo jioni ya siku hiyo watacheza mechi nyingine ya
kirafiki dhidi ya Ndanda fc katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
“Tayari tuna timu kutoka Uganda. Hii itakuwa ni
mechi ya kimataifa na mechi yetu ya mwisho ya kimataifa ya kirafiki kabla ya
kuanza kwa ligi”
“Tunatarajia kucheza siku ya Ijumaa saa 11:00
jioni, lakini vilevile jumamosi tutakuwa kule Mtwara na baada ya hapo timu itarudi
Dar es salaam kwa maandalizi zaidi ya mwisho”. Alisema Kaburu.
“Awali tulikuwa tumeomba timu kutoka Rwanda, APR
lakini wamechelewa kuthibitisha na hawataweza kufika kwasababu wanaandaa timu
yao”.
“Mwalimu (Phiri) aliomba mechi mbili za kimataifa
za kirafiki, hivyo wenzetu hawa wa Uganda URA wamethibitisha kuja na kesho
watakuwa hapa Dar es salaam”.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba walicheza mechi
ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki chini ya Patrick Phiri dhidi ya Gor Mahia ya
Kenya na kushinda mabao 3-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na mshambuliaji mpya,
Paul Kiongera na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Licha ya ushindi huo, Simba ilicheza soka safi
lililowavutia mashabiki wake na kuamini msimu ujao watacheza kwa kiwango cha
juu.
Simba wataanza kampeni ya kusaka ubingwa wa ligi
kuu Tanzania bara septemba 21 mwaka huu dhidi ya Coastal Union uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.