Headlines
Published On:Alhamisi, 11 Septemba 2014
Posted by Hisia

SIMBA KUCHEZA NA URA HALAFU NDANDA FC NDANI YA SAA 24, UNADHANI NI DHARAU KWA WANAMTWARA?

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


SIMBA SC kesho ijumaa inacheza mechi ya pili ya kimataifa ya kirafiki chini ya kocha Patrick Phiri dhidi ya timu ya mamlaka ya ukusanyaji wa mapato nchini Uganda, URA katika uwanja wa Taifa jijini Dar es slaam.
Mechi hiyo itaanza majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika mashariki.
Wakati huo huo jumamosi jioni, Simba itakuwa na mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Ndanda fc katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara katika maadhimisho ya ‘Ndanda fc Day’.
Watu wengu hususani wa Mtwara wanahoji inakuwaje Simba wanacheza mechi kesho wakati Jumamosi wanatakiwa kuwa Mtwara?, wachezaji wataweza kumudu mechi mbili ndani ya saa 24?
Walio wengi wanaonesha wasiwasi juu ya ufanisi wa Simba katika mechi ya Mtwara na kuona kama hawajaichukulia kwa uzito wa juu.
Kwa faida ya wasomaji, Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange Kaburu alisema jana kuwa awali waliomba mechi na APR ya Rwanda ambao walichelewa kuthibitisha kwasababu wana majukumu mengine ya kuiandaa timu yao.
Baada ya hapo wakawasiliana na URA ambao walithibitisha kuja nchini kucheza na Simba na watawasili leo uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere , jijini Dar es salaam.
Kaburu alisema kikosi kizima cha Simba kitaondoka jumamosi asubuhi kwa Ndege kwenda kucheza mechi Mtwara jioni ya siku hiyo. Awali ilitakiwa Simba wasafiri Ijumaa kwenda kuwafuata Ndanda.
Kwa wale wanaohoji, kiufundi, mechi ya kimataifa ya kirafiki ya kesho dhidi ya URA ina umuhimu mkubwa zaidi kwa viongozi wa Simba kwasababu tayari kocha mkuu Phiri aliomba apate mechi mbili za kujipima nguvu.
Kama wasingepata mechi ya pili ya kimataifa baada ya kuifunga Gor Mahia mabao 3-0 uwanja wa Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita, ingekuwa dosari na kosa la kwanza kumkosea Phiri aliyewaambia mapema kabisa.
Kutokana na mapendekezo ya Phiri, viongozi wamekuwa wakihaha kupata timu na hatimaye kuipata URA.
Hivyo mechi hiyo ni muhimu zaidi kuliko kuitegemea ya Mtwara. Sio kwamba Ndanda fc sio kipimo kizuri, hapana, ni kizuri tu, lakini URA ni kizuri zaidi.
Kiufundi, Phiri anajua wazi kuwa anatakiwa kupata mechi ngumu za kujipima nguvu ili kujua makosa yako wapi.
Kuna namna mbili za kuipima timu. Kuna wakati kocha anatafuta mechi nyepesi ili kuona namna wachezaji wake walivyomuelewa.
Kama wachezaji wako wamewazidi wapinzani kwa kila kitu, kama mwalimu, inakuwa rahisi kujua kama mfumo wako unafanya kazi na wanaelewa maelekezo. 11111
Ukimzidi mpinzani, una nafasi kubwa ya kuonesha uwezo mkubwa kimbinu na kiufundi, na ndio maana makocha wakati fulani wanatafuta mechi nyepesi.
Unaweza kuponda kwanini kocha anapendekeza mechi nyepesi sana? Anaogopa changamoto au?
Wenye taaluma na ukocha wanafahamu umuhimu wa mechi rahisi pale unapotaka kuona ubora wa timu yako katika kutekeleza mfumo uliopandikiza.
Jaribu kufikiria, mara nyingi duniani kote makocha wanaanza mechi za kirafiki rahisi, na kadri wanavyofanya mazoezi kwa muda mrefu wanaongeza timu ngumu na kama wana muda wa kutosha wanacheza na timu ngumu zaidi.
Malengo ni yale yale, wanataka kuona maendeleo ya vikosi vyao kwa mujibu wa maelekezo wanayoyatoa kulingana na falsafa zao.
Pili; makocha wanajaribu timu zao kwa kucheza mechi ngumu za kirafiki. Hii inamsaidia kuona kama wachezaji wake wanamudu changamoto.
Kama mpinzani wako ni bora zaidi, inawapa ugumu wachezaji  wako kucheza vile utakavyo na kuna wakati inawalazimu kutumia vipaji binafsi kuliko maelekezo ya mwalimu.
Mchezaji akizidiwa lazima utafute mbinu mbadala pale za mwalimu wake zikifeli. Kuwapima wachezaji wako na wapinzani bora, ni njia rahisi ya kujua mapugufu ya kikosi chako.
Leo hii huwezi kuipima safu ya ulinzi kwa kutumia timu nyepesi ambayo katika mchezo mzima inapiga mashuti mawili tu golini. Utakuwa unajidanganya. Lazima utafute timu ngumu, yenye washambuliaji wazuri, na hii itafichua udhaifu.
Patrick Phiri alianza kwa kucheza mechi za kirafiki visiwani Zanzibar na kushinda zote, akaona kuna haja ya kuwapima na timu ngumu zaidi. Simba wakacheza na Gor Mahia ya Kenya na kushinda.
Kuna makosa yawezekana mwalimu aliyaona na akaona kuna haja ya kuongeza mechi nyingine baada ya kufanyanyia kazi katika mazoezi, na ndio maana kapewa URA .
Kutokana na mazingira ya Simba na namna wanavyotaka kufikia malengo ya ubingwa msimu ujao, mechi ya kesho ni muhimu zaidi kwao.
Ingawa kwa upande wa Ndanda fc wanaweza kukerwa na hili, lakini ni mechi yenye msaada wa kimbinu na kiufundi kwa Patrick Phiri.
Inawezekana Ndanda watatoa changamoto nzuri kwa Simba, lakini haiwezi kulingana na URA kutokana na uzoefu wao na aina ya wachezaji waliopo.
Naamini Simba wana kikosi kikubwa na wanaweza kupata timu mbili zenye ubora wa juu. Kule Zanzibar, Phiri alikuwa anabadilisha karibu kikosi kizima.
Kama Ivo Mapunda hatacheza jumamosi Mtwara, hata Hussein Sharrif ‘Casillas’ atakuwa kipimo kizuri kwa washambuliaji wa Ndanda kwasababu ndiye kipa bora wa msimu uliopita.
Ndanda fc wameeleza wazi kuwa mchezo dhidi ya Simba ni mechi yao ya mwisho kubwa kabisa ya maandalizi. Wanaiheshimu Simba wamejua ni kipimo kizuri kwao.
Kwa aina ya wachezaji wa Simba, yeyote atakayeanza, itakuwa changamoto nzuri kwa Ndanda. Waliowengi ni wazoefu na mechi za ligi kuu, hata kama hawana umri mkubwa.
Kwa watu wa Mtwara mnaouliza kwanini Simba wamefanya hivyo, nadhani nimejaribu kueleza kwa kifupi kwanini wamefikia maamuzi hayo ya kucheza mechi mbili ndani ya saa 24.

About the Author

Posted by Hisia on 9/11/2014 09:06:00 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

By Hisia on 9/11/2014 09:06:00 PM. Filed under , . Follow any responses to the RSS 2.0. Leave a response

0 comments for "SIMBA KUCHEZA NA URA HALAFU NDANDA FC NDANI YA SAA 24, UNADHANI NI DHARAU KWA WANAMTWARA?"

Leave a reply

    Blog Archive