Published On:Jumanne, 9 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA “MACHO KWA MACHO’ NA NDANDA FC WIKIENDI, MTWARA HOMA YAANZA KUPANDA!
Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Simba kitakabiliana na Ndanda fc katika mechi ya kirafiki
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba chini ya kocha Mzambia,
Patrick Phiri, wameanza tena mazoezi ya kujiwinda na ligi kuu Tanzania bara
katika uwanja wa Boko Veterani, jijini Dar es salaam baada ya kucheza mechi ya kimataifa
ya kirafiki mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Katika mechi hiyo iliyovuta hisia za mashabiki
wengi, Simba walicheza soka maridadi, wakitandaza mpira chini, pasi za uhakika
na mashambulizi ya kupangika.
Mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera alifunga mawili
na Ramadhani Singano ‘Messi’ moja na
kuipa Simba ushindi wa mabao 3-0.
Kabla ya mechi hiyo, Simba waliweka kambi visiwani
Zanzibar ambapo walicheza mechi kadhaa za kirafiki na kushinda zote.
Ikiwa ni sehemu ya kuendelea kujiweka sawa, Makamu
wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema Simba itakuwepo Dar es salaam
badala ya kurejea Zanzibar kama ilivyopangwa awali na itaondoka Ijumaa kwenda
Mkoani Mtwara kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ndanda fc.
Mechi hiyo muhimu kwa Phiri itachezwa katika
uwanja wa Nangwanda Sijaona ambao utazinduliwa siku hiyo baada ya kufanyiwa
marekebisho makubwa kwa ajili ya ligi kuu msimu ujao.
Baada ya mechi ya Mtwara, Mnyama atarejea Dar es
salaam kuendelea na programu ya mazoezi kujiandaa na mchezo wa ufunguzi wa ligi
kuu bara dhidi ya Coastal Union, Septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam.
Ili kuwaweka vijana wa Patrick Phiri katika
mazingira mazuri zaidi na tulivu, Mnyama anaingia kambini katika Hoteli ya
Shynovo, maeneo ya Africana, Mbezi, Beach, Dar es salaam tayari kwa mawindo ya
ligi kuu.
Kwa upande wa Ndanda fc wamesema wanaendelea
vizuri na mazoezi yao na wamefurahi kupata mechi ngumu ya kirafiki dhidi ya
Simba sc.
Katibu mkuu wa Ndanda fc, Seleman Kachele amesema
kikosi kizima cha timu yao kinasafiri kesho kutokea Dar es salaam kwenda
Mtwara.
Jumapili ya wiki iliyopita, Ndanda fc ilipigwa bao
1-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa
kirafiki uliopigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
“Sisi tuko Dar es salaam na tunaondoka kesho
kwenda Mtwara kwa ajili ya hiyo mechi. Maandalizi yanakwenda vizuri na hiyo ni
mechi yetu kubwa ya kirafiki ya kujipima nguvu kabla ya kuanza ligi kuu”.
“Kuna kasoro mbalimbali kwenye kikosi na ndio
maana tumekuwa tukimtafutia mwalimu mechi kubwa za kirafiki baada ya kufungwa
1-0 na Mtibwa Sugar.
“Tunaamini tukicheza na Simba itakuwa nafasi nzuri
kwa mwalimu kujua makosa yake na kuyafanyia kazi. Simba ni timu kubwa, ilishika
nafasi namba 4 katika ligi. Watatupa changamoto hasusani ukabaji na kikosi
kitakachotumika ndicho kitakuwa cha ligi kuu”.
Septemba 20 mwaka huu, Ndanda fc wataanza ugenini
kampeni za ligi kuu kwa kuivaa Stand
United katika uwanja wa Kambarage.
Simba wao wataanza na Coastal Union septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.