Published On:Jumamosi, 13 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA NA NDANDA FC, ZATOKA BILA KUFUNGANA - NANGWANDA SIJAONA MTWARA
Kikosi cha Simba kilichoanza leo dhidi ya Ndanda fc uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara
SIMBA SC chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri
imeshindwa kutamba mbele ya Ndanda fc na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana (0-0) katika mchezo wa kirafiki uliopigwa jioni
hii uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Hii ni mechi ya pili kwa Simba ndani ya saa 24 ambapo
jana uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ilifungwa bao 1-0 na URA ya Uganda
katika mechi ya kimataifa ya kirafiki.
Kabla ya hapo, Simba waliibuka na ushindi wa mabao
3-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, wikiendi iliyopita uwanja wa Taifa jijini Dar
es salaam.
Mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera alifunga mawili
na Ramadhani Singano ‘Messi’ alifunga moja.
Katika mechi hizo mbili za kimataifa, Mfungaji
bora wa msimu uliopita, Mrundi, Amissi Tambwe hakucheza, lakini leo alianzishwa
na kocha Phiri, ingawa alishinda kuziona nyavu.
Kikosi cha Ndanda fc kilichoanza dhidi ya Simba sc
Kwa ujumla mechi ya leo huko Mtwara ilikuwa nzuri
na vijana wa Ndanda walicheza kwa kiwango kizuri, hivyo kuwa kipimo sahihi kwa
Simba sc.
Simba nao walionesha soka zuri na kuifanya mechi
kuwa 50-50, lakini hawakuwa na ujanja wa kuwafunga Ndanda fc walioshuhudiwa na
umati mkubwa wa mashabiki wao.
Uwanja wa Nangwanda ulifurika mashabiki ambao
walikuwa na hamu ya kuiona Simba ikiwa ni miaka mingi imepita bila kuona klabu
kubwa ya ligi kuu ikicheza mkoani humo.
Simba walicheza mbele ya Rais wao, Evans Elieza
Aveva ambaye jana aliongozana na mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Hassan Dalali
kuzindua tawi la Simba mkoani Mtwara.
Rais wa Simba sc, Evans Elieza Aveva (wa kwanza kushoto, wanaotembea) akiingia Jukwaa kuu
Mechi hii ni ya mwisho ya majaribio kwa kocha
Phiri na kikosi chake kinarejea Dar es salaam kabla ya kurudi tena kambini
Visiwani Zanzibar kumalizia program ya maandalizi yake.
Simba wataanza ligi kuu septemba 21 uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam kwa kuwakabili wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Wakati wao Ndanda fc watasafiri mpaka uwanja wa
Kambarage mkoani Shinyanga kuwavaa wenyeji Stand United, septemba 20 mwaka huu.