Published On:Ijumaa, 19 Septemba 2014
Posted by Hisia
MADAKTARI WAZISHITAKI SIMBA, MBEYA CITY
Simba na Mbeya City zipo hatarini
kupanda kizimbani kujibu shitaka la kukiuka kanuni na sheria za Fifa, kwa
kitendo cha kutopima afya za wachezaji kabla ya kuanza kuzitumikia kwa msimu
ujao.
Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa) zinaeleza kuwa, kila mchezaji ni lazima afanyiwe vipimo vya afya kabla
ya kuanza kucheza, agizo ambalo linaonekana kutokuwa na mashiko nchini
Tanzania.
Katibu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba za
Michezo Tanzania (Tasma), Nassor Matuzya, ambacho ndicho kinahusika na upimaji
wa afya za wachezaji nchini, amesema mpaka jana Alhamisi ni timu tano tu ndizo
zilikuwa zimetekeleza kanuni hiyo ambazo ni Yanga, Azam, Coastal Union, Mgambo
na Ndanda huku Panone FC ikiwa ni timu pekee kutoka Ligi Daraja la Kwanza.
Matuzya, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Tiba
ya TFF, amekwenda mbali na kusema Simba walipewa taarifa mara mbili lakini
hawajatekeleza.
“Tunawashtaki kwa BMT (Baraza la Michezo la
Tanzania) na baadaye tunaweza hata kuwafikisha mahakamani,” alisema daktari
huyo wa zamani wa Yanga.