Published On:Jumatatu, 15 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA WARUDI ZENJI TENA KUTAFUTA ‘DAWA’ YA LIGI KUU
Kikosi cha Simba sc kilichokwenda Mtwara jumamosi na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana (0-0) dhidi ya wenyeji Ndanda fc
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi , Simba SC, wanaenda kuweka
kambi tena Visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya ligi kuu soka
Tanzania bara inayotarajia kuanza
kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Simba chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri
wataanza kampeni za kusaka ubingwa walioukosa kwa misimu miwili dhidi ya Wagosi
wa Kaya, Coastal Union, septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa , Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘kaburu’ Perez
amesema: “Leo timu inaelekea Zanzibar
kwa ajili ya mkakati wa mwisho wa kujiandaa na ligi kuu na jumamosi timu
itarudi Dar es salaam kwaajili ya mchezo wa jumapili dhidi ya Coastal Union
uwanja wa Taifa.”
Hii itakuwa mara ya pili Simba kujificha Zanzibar
kwasabababu ilikuwa huko kabla ya kuja Dar es salaam kucheza mechi ya kirafiki
dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, septemba 6 mwaka huu uwanja wa Taifa.
Katika mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki, mabao
mawili ya Paul Kiongera na moja la Ramadhani Singano ‘Messi’ yalitosha kuwapa
Simba ushindi wa 3-0.
Baada ya mechi hiyo, Simba waliendelea kubakia Dar es salaam badala
ya kurudi Zanzibar kama ilivyokuwa imeelezwa awali na alikuwa inafanya mazoezi
katika uwanja wa Boko Veterani.
Ijumaa ya wiki iliyopita, Simba ilicheza mechi ya
pili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda na kulala bao 1-0.
Kesho yake (jumamosi) ya wiki iliyopita, Simba
ilisafiri kwenda Mtwara ambapo ilicheza mechi ya kirafiki na Ndanda fc katika
uwanja wa Nangwanda Sijaona na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana.
Baada ya mechi hiyo, jana wachezaji walipewa
mapumzikio, na leo jumatatu wanaanza mazoezi kabla ya kuelekea Zanzibar.
Simba wamekuwa wakiijenga timu upya chini ya kocha
Phiri na usajili wao unawafanya wapinzani wawe na wasiwasi.
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba wameonekana kuwa
na ubora wa kutosha, hivyo kujenga imani kwa mashabiki wao.
Warundi, Amissi Tambwe, Pierre Kwizera, Mkenya,
Paul Kiongera na Waganda Joseph Owino na Emmanuel Okwi wameonekana kuwa na
msaada mkubwa kwa Simba.
Pia wapo wazawa waliosajiliwa kama, kipa Hussein
Sharrif, Shaaban Kisiga, Elius Maguli,Joram Mgeveke, Tshabalala, na wengineo.
Wachezaji hawa wameonakana kuelewana na kucheza mpira mzuri kama walivyoonekana kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia na URA.