Published On:Ijumaa, 12 Septemba 2014
Posted by Hisia
SIMBA YAVUNJA REKODI YA YANGA KUWANIA WACHEZAJI
Emmanuel Okwi
REKODI zinaonyesha
kwamba Simba haijawahi kushinda kesi ya kumwania mchezaji yeyote kati
yake na Yanga au Costal Union kwa takribani miaka 20.
Mara kadhaa timu hiyo
yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam imejikuta
ikibwagwa katika vita ya kugombea mchezaji kati yake na klabu hizo, lakini
hukumu za wachezaji Emmanuel Okwi na Abdul Banda zilizotolewa na Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF Jumapili iliyopita kwa mara ya kwanza
imewapa Simba ushindi dhidi ya Yanga na Coastal Union.
Hapa chini ni baadhi ya
wachezaji ambao wamewahi kugombewa na timu hizo dhidi ya Simba.
Mtemi
Ramadhani Mwaka 1980;
Simba ilimgombea
kiungo huyo na Yanga. Mchezaji huyo alikuwa akichezea Waziri Mkuu ya
Dodoma lakini alijikuta akisajili katika timu za Simba na Yanga.
Akiwa na Taifa Stars
iliyokuwa imekwenda Nigeria kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
(Afcon), Mtemi alizua balaa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati Stars
walipokuwa wakirejea.
Viongozi wa Simba na
Yanga na wale Pan African walikuwa kiwanjani hapo kuwalinda wachezaji
waliowasajili na kuwafanya washikane mashati.
Mbali na Mtemi,Yanga pia
walikuwa wakimgombea, Rashid Idd ‘Chama’ waliokuwa wamemsajili wao pamoja
na Pan African.
Chama cha Mpira wa Miguu
(FAT, sasa TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Said El Maamry waliwawataka
wachezaji hao kuchagua timu za kuchezea.Mtemi alichagua kuchezea Simba na Chama
aliichagua Pan African lakini Yanga hawakukubali wakakata rufaa Baraza la
Michezo Tanzania (BMT).
BMT iliamua kuwafungia
wachezaji hao kwa mwaka mmoja, baada ya hapo Mtemi alirudi Waziri Mkuu na baada
ya msimu mmoja akajiunga na Simba. Chama naye aliendelea kuchezea Pan African.
Yussuf
Bana; Mwaka 1981
Simba ilimgombea beki
Yussuf Ismail Bana katika vita na Yanga. Beki huyo alicheza Simba msimu
mmoja tu na kuamua kujiunga na Yanga mwaka 1982 kitu kilichozua utata mkubwa.
Inadaiwa, Yanga ilimsajili kwa jina lake halisi la Yussuf Ismail na Simba
walimsajili kwa jina la Yussuf Bana ambalo lilidaiwa kuwa ni jina la la
utani.
Baada ya vita ya
chinichini hatimaye, Bana ambaye kwa sasa ni marehemu aliruhusiwa kuchezea
Yanga.
Francis
’Fura’ Mwikalo;
Simba ilipoteza
matumaini ya kunyakuwa ubingwa wa Tanzania Bara mwaka 1985/86 baada ya
kumsajili mchezaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, Francis Mwikalo.
Katika kutaka kuonyesha
kwamba mchezaji huyo alikuwa ni tofauti na Mwikalo wa Coastal Union, Simba walimbadilisha
jina na kumsajili kwa jina la Fura Mwikalo.
Sakata la mchezaji huyo
lilikuwa kubwa sana na kufikia hatua ya kuamuliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
wa Kisutu jijini Dar es Salaam. Siku ya hukumu, mashabiki, wapenzi na wanachama
wa Simba walifika mahakamani wakiwa na ngoma ya Kizaramo aina ya
Mdundiko wakiamini kwamba watashinda kesi hiyo na kutangazwa kuwa mabingwa.
Baada ya hukumu kutolewa
na Simba ilibwagwa na kupoteza pointi zote walizomchezesha Mwikalo ambaye awali
walidai kuwa walimsajili kutoka Muheza Shooting ya Tanga.
Athuman
Idd ‘Chuji’;
Yanga iliiwaduwaza
tena watani zao kwa kumnyakuwa beki wa zamani wa Polisi Dodoma, Athumani
Idd Chuji ambaye aliikacha Simba katika hatua za mwisho mwaka 2006.
Pamoja na Mwenyekiti wa
Simba wakati huo, Hassan Dalali kudai kwamba Chuji hatacheza soka, mchezaji
huyo alisema ni heri akauze ndimu kuliko kurudi Simba. TFF ilimwidhisha
kuchezea Yanga.
Mbuyu
Twite;
Agosti, 2012
aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisafiri kwenda DR Congo kumsajili
beki Mbuyu Twite. Hata hivyo, Yanga waliwazidi akili na kumsajili beki kwa kile
kilichoelezwa kwamba Simba walishindwa kufuata sheria za usajili.
Simba ilidaiwa
kukurupuka bila ya kufuata sheria za CAF na Fifa, hivyo TFF kumwidhinisha
kuchezea Yanga.
Kelvin
Yondani;
Mwaka huohuo,
Simba ilipata pigo lingine kubwa baada ya beki wake wa kati Kelvin Yondani
kusajiliwa na Yanga.
Awali, Yondani aliondoka
Simba na kwenda kujichimbia Mwanza ambako alipoibuka alitua Jangwani kwa
dau la Sh30 milioni.
Pamoja Rage kudai kwamba
Yondani asingeweza kucheza soka TFF ilimwidhinisha mchezaji huyo kukipiga
Yanga.
Mrisho
Ngassa;
Baada ya kumchukua kwa
mkopo kutoka Azam, Simba walimwongezea Ngassa usajili wa mwaka mmoja na kumpa
gari pamoja na Sh25 milioni.
Msimu wa kutolewa kwa
mkopo Simba ulipoisha, Yanga ilimsajili Ngassa kwa ada ya Dola 30,000.Simba
hawakukubali, lakini TFF ilimwidhinisha Ngassa kuchezea Yanga na kumtaka
kurudisha fedha za Simba alizopewa, piaalifungiwa michezo sita.
Iliwabidi Simba kusubiri
hadi Jumapili iliyopita kuibadili kibao.
Chanzo: Mwanaspoti