Published On:Jumanne, 9 Septemba 2014
Posted by Hisia
TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA MWAMUZI LUGENGE
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mwamuzi wa daraja la
kwanza (class one), Luteni David Lugenge kilichotokea jana (Septemba 7
mwaka huu) kwa ajali ya gari katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Luteni Lugenge
ambaye mwishoni mwa wiki alishiriki mitihani ya utimamu wa mwili kwa
waamuzi wa Ligi Kuu alikuwa na ndugu yake Christopher Alexander Lunyungu
katika gari dogo wakienda mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Handeni, Peter Juma,
Luteni Lugenge alikuwa akimsindikiza mwenzake aliyekuwa anakwenda
kujitambulisha kwa wakwe zake watarajiwa.
Msiba huo ni
mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Luteni Lugenge alikuwa ni
mmoja wa waamuzi wanaoinukia nchini, hivyo mchango wake ulikuwa bado
unahitajika. Hivyo tutamkumbuka daima.
TFF tunatoa pole
kwa familia ya marehemu Luteni Lugenge, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa
Miguu nchini (FRAT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka
kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito.
BONIFACE WAMBURA
KNY KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)