Published On:Ijumaa, 12 Septemba 2014
Posted by Hisia
PAUL KIONGERA ATAING`ARISHA SIMBA TENA?
Mkali wa sarakasi, Paul Kiongera akishangilia bao lake la pili dhidi ya Gor Mahia wikiendi iliyopita
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
PAUL Kiongera ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya
vizuri kwa sasa katika kikosi cha wekundu wa Msimbazi Simba chini ya kocha
Patrick Phiri.
Mkenya huyu alitua katika rada za Simba chini ya
mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe majira ya kiangazi mwaka
huu akitokea nchini Kenya.
Jina lake lilipata umaarufu zaidi baada ya kutokea
benchi wikiendi iliyopita na kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0
waliopata Simba dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Mechi hii ya kimataifa ya kirafiki ilikuwa ya kwanza
kwa Phiri tangu arejee kuinoa Simba na leo hii anacheza mechi ya pili ya
kimataifa dhidi ya URA ya Uganda.
Wachezaji wa Simba watapata nafasi ya kuwaonesha
mashabiki wao kuwa wamejiandaa vizuri wakati huu wa mapinduzi klabuni hapo.
Kiongera kama ataonesha uwezo mkubwa kwa mara
nyingine, basi atawashika zaidi mashabiki wa Simba wenye kiu ya mafanikio.
Watatisha?: Wachezaji wa Simba wakishangilia goli la Singano kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia jumamosi iliyopita
Naye Ramadhani Singano ‘Messi’ baada ya kufunga
moja dhidi ya Gor Mahia, ataonesha kiwango kile kile au ataongeza? Dakika 90
zitadhihirisha.
Katika mechi dhidi ya Gor Mahia, Simba walicheza
vizuri hususani kipindi cha pili ambapo Safu ya kiungo ilishirikiana vizuri na
safu ya ushambuliaji.
Wachezaji kama Uhuru Seleman, Shaaban Kisiga,
Awadh Juma, Ramadhani Singano, Paul Kiongera walionekana kuelewana zaidi na
kuifanya Simba icheze mpira wake uliopotea kwa muda mrefu.
Walijitahidi kuweka mpira chini, pasi za haraka
haraka na za uhakika na kupanga mashambulizi vizuri na hatimaye kupata magoli
matatu.
Gor Mahia ambao hawakuonekana kipindi cha pili
walijitahidi kushambulia, hususani kipindi cha kwanza, lakini kipa Ivo Mapunda
na mabeki wake kama Joseph Owino, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ walicheza kwa
kiwango cha juu, wakikaba na kuzuia mianya ya wapinzani kumfikia Ivo.
Je, baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Gor Mahia,
leo itakuwaje? Dakika 90 zitatoa jibu.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
amesema maandalizi kwa ajili ya mechi ya leo yamekamilika, mambo ya usalama
yako safi, hivyo ni fursa ya mashabiki kufurika kuitazama timu yao.
Kaburu alisema wameandaa utaratibu mzuri wa kuuza
tiketi ambapo zitaanza kuuzwa leo kuanzia saa 4:00 asubuhi katika magari
maalumu yaliyoandaliwa sehemu mbalimbali.
Mbali na mechi ya leo, Kaburu aliongeza kuwa Simba
wana mwaliko maalumu kutoka Ndanda fc ili washirikiane kuadhimisha siku ya ‘Ndanda
fc Day’ kesho jumamosi.
“Tayari tumeandaa utaratibu mzuri, kikosi kizima
cha Simba kikiwa na benchi la ufundi, jumamosi asubuhi, wote watakwenda Mtwara
kwa usafiri wa Ndege”
“Siku hiyo jioni tutakuwa pamoja na watu wa Ndanda katika siku yao na kucheza mechi moja ya kirafiki ambayo itakuwa ya mwisho kwetu ya maandalizi na jumatatu tutarudi kambini Zanzibar kabla ya kuanza kwa ligi kuu”. Alisema Kaburu.