Published On:Jumatatu, 8 Septemba 2014
Posted by Hisia
HUU NDIO UJANJA WA OKWI, AMFANYA HANS POPPE AWAPIGE BAO LA KISIGINO YANGA SC
Mkali
wa sheira?: Emmanuel Okwi (kulia) akiwaonesha ufundi wachezaji wa Gor
Mahia siku ya jumamosi uwanja wa Taifa, Simba ikishinda 3-0
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KAMA ubongo wako una uwezo mzuri wa kutunza
kumbukumbu, Ijumaa ya Agosti 29 mwaka huu klabu ya Young Africans ilitangaza kumshitaki
mchezaji Emmanuel Okwi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuwasilisha
nakala kwa shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) na shirikisho la soka duniani
(FIFA) kwa kuingia mkataba na timu nyingine wakati akiwa bado ana mkataba wa
miaka miwili.
Mwenyekiti wa Yanga,
Yusuf Manji aliwaambia waandishi wa habari siku hiyo kuwa uongozi wa klabu huyo
ulishangazwa na kitendo cha viongozi Simba , wakala na mchezaji mwenyewe kuingia mkataba wa miezi
sita kwa madai kuwa anataka kulinda kiwango chake wakati akiwa na kesi na
Yanga.
Manji alisema awali Yanga walipeleka malalamiko
TFF na kuwapa nakala CAF na FIFA kuwa Emmanuel Okwi awali alifanya mazungumzo
na timu ya Wadi Degla FC ya nchini Misri na kufikia klabu hiyo kutuma ofa ya
kutaka kumnunua bila kuwasiliana na uongozi wetu.
Wakati Yanga
wakisubiri majibu kutoka TFF wakashangaa kuona mchezaji huyo amesaini mkataba
mwingine, na wakadai mchezaji huyu alikuwa akirubuniwa na watu na kufikia hatua
ya kusaini mkataba mwingine kitu ambacho
alikiuka sheria za FIFA za usajili.
Baada ya kuona amesaini
mkataba na Simba, Yanga walichokifanya ni kuandika barua nyingine TFF juu ya
suala hilo na kuomba kulipwa fidia ya US Dollar 500,000 (sawa na TZS
800,000,000/=) kutoka kwa klabu ya Simba, wakala wake na mchezaji mwenyewe.
Aidha uongozi wa
Yanga uliomba TFF kulipatia ufumbuzi suala hilo ndani ya siku saba, na kama
siku saba zikikipita basi uongozi wa Jangwani utakwenda moja kwa moja FIFA na
ikishindakana mahakama ya soka CAS, lakini hilo halikufanyika hata kama TFF
hawakutelekeza ndani ya siku hizo saba.
Amechemsha?:
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji (kulia) siku alipotangaza kumshitaka
Okwi. Kushoto ni makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga.
Yanga waliongeza kuwa
lengo lao halikuwa kuikomoa timu ya Simba, bali walichotaka ni sheria ifuatwe,
kwani Okwi alikua ameitumikia klabu ya Yanga kwa kipindi cha miezi sita tu, na
kuwa amebakiza mkataba wa miaka miwili mpaka mwishoni mwa 2015/2016.
Sheria iko wazi
kabisa mchezaji anayekutwa na kosa la kusaini sehemu mbili adhabu yake ni
kufungiwa kucheza soka kuanzia mwaka mmoja na kuendelea huku klabu husika
ikifungiwa kusajili kuanzia miaka mwili na kuendela na kushushwa daraja au
adhabu zote kwa pamoja.
Jana (septemba 7 mwaka huu), kamati ya Sheria na
Hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la soka Tanzania TFF ilikutana kujadili
mgogoro huo wa kimkataba baina ya Okwi na klabu yake ya Yanga.
Kamati ilisema kilichokuwa kikijadiliwa sio
usajili wa Okwi bali ni suala la kimkataba.Kwa maana hiyo, Simba haikujadiliwa
hata kidogo, bali ni Okwi na Yanga.
Katika kikao cha jana, mkataba huo ulipitiwa
vizuri, mchezaji akasikilizwa na upande wa Yanga nao wakapewa nafasi, lakini
mwisho wa siku ikabainika kuwa mkataba baina ya pande hizo mbili umevunjika,
kwa mujibu wa kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji.
Kwanini umevunjika? Jibu likawa rahisi sana. Ukiwa
ni mkataba wa pande mbili, Yanga akiwa mwajiri, alikiuka kipengele cha 8 kuhusu
malipo ya ada ya usajili.
Wametengana: Emmanuel Okwi (kulia) alicheza na Mganda mwenzake, Hamis Friday Kiiza wakiwa Yanga sc msimu uliopita.
Yanga haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba
hadi kufikia juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba uvunjwe.
Kutokana na hilo, Okwi ni mchezaji huru na anaruhusiwa
kujiunga na klabu yoyote ikiwemo Simba ambapo amesaini mkataba wa miezi sita.
Stori ya Okwi iliteka hisia za mashabiki wengi wa
mpira wa miguu nchini kwasababu ilihusisha klabu mbili kongwe, Simba na Yanga.
Mara kadhaa klabu hizi zinapigana vikumbo katika
usajili na kama una kumbuka usajili wa Mbuyu Twite Jr ulizifanya klabu hizi
zivutane vikali, lakini mwisho wa siku Yanga wakaibuka videdea.
Safari hii Simba hakuwa na tatizo lolote na Yanga
kwa mujibu wa maelezo ya hapo, lakini Okwi alikuwa na tatizo na Yanga. Kutokana
na upinzani mkubwa wa klabu hizi kongwe, Simba nao walikuwa wakizungumzwa
mtaani kama wameifanyia kitu mbaya Yanga juu ya mchezaji huyo.
Kumbe kisheria haikuwa hivyo. Okwi na Yanga ndio
walikuwa wanapambana.
Pia kulikuwa na pingamizi la Coastal Union juu ya
usajili wa Abdi Banda kujiunga na Simba. Coastla walidai bado wana mkataba wa
miaka miwili na Banda na walitangaza kumfungia mwaka mmoja kucheza soka kwa
kitendo cha kusaini mikataba miwili.
Kumbe Coastal nao walikiuka kipengele cha
kimkataba ambapo walishindwa kumlipa mchezaji mshahara wa miezi mitatu
mfululizo kama takwa la mkataba linavyotaka.
Abdi Banda naye aliwekwe pingamizi na Coastal unioni, lakini kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF imemsafisha.
Coastal Union iliwakilishwa na kiongozi mmoja
wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Tofauti ya Okwi na Banda ni ndogo tu, lakini kwa
asilimia kubwa sakata lao linafanana.
Yanga walishindwa kutimiza malipo ya ada ya
usajili kama takwa la kimkataba, wakati Coastal walishindwa kumlipa mchezaji
mshahara kama takwa la mkataba linavyosema.
Ukiangalia masakata haya mawili, kuna watu
walishindwa kutimiza majukumu yao kwa upande wa Yanga na Coastal Union.
Mkataba ni suala la kuheshimika. Kila kipengele
kina maana kubwa na kushindwa kutekeleza kimoja tu au sehemu ndogo ya mkataba
unaweza kupoteza haki yako.
Yanga kwa kushindwa kutekeleza kipengele cha 8
kuhusu malipo ya ada ya usajili wamepoteza haki ya kummiliki Okwi aliyebakiza miaka
miwili katika mkataba wake, hali kadhalika Coastal Union kwa Banda.
Kuna picha inanijia kichwani mwangu kuwa klabu
kubwa za hapa nchini hazina mfumo mzuri wa kusimamia mikataba yao na hata
uvunjwaji wa mikataba ya wachezaji unakuwa na mapungu mengi.
Hii pia inachangiwa na ueledi mdogo wa wachezaji
wa soka la Bongo katika masuala ya mikataba. Leo hii ukiuliza ni wachezaji
wangapi wana wanasheria wao?Jibu ni wachache tu. Na ndio maana viongozi wa
Yanga na Simba na klabu nyingine wanakuwa na jeuri ya kujivunjia mikataba na
hawalipi haki za wachezaji.
Ameshinda? : Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe
Kuna lundo kubwa la wachezaji wamevunjiwa mikataba bila kulipwa haki, lakini kwakuwa wengi ni “mambumbu’ wamekaa na kulia kilio cha samaki. Samahani kwa neno hili, lakini inabidi nilitumie tu.
Kuna lundo kubwa la wachezaji wamevunjiwa mikataba bila kulipwa haki, lakini kwakuwa wengi ni “mambumbu’ wamekaa na kulia kilio cha samaki. Samahani kwa neno hili, lakini inabidi nilitumie tu.
Unakumbuka sakata la John Njoroge, Wisdom Ndlovu
na Yanga au kocha Papic na Yanga? Ilikuwa ni madhara ya kuvunja mkataba
kiholela.
Hata Simba nao walishawahi kuingia kwenye matatizo
ya kuvunja mikaba na wachezaji bila kuwalipa haki zao. Lipo kundi kubwa la
wachezaji hao, lakini sitalitaja kwa leo.
Ukiangalia suala la Okwi, sio gumu kabisa. Mganda
huyu ana akili nyingi na anazifahamu vizuri sheria za kimkataba. Hata kama sio
yeye binfasi, basi nyuma ana washauri wazuri wa kisheria.
Anapoamua kitu ujue anajua kwa kutokea. Unakumbuka
sakata la Okwi na Etoile Du Sahel ya Tunisia?
Simba ilimuuza Okwi kwenda klabu hii kwa zaidi ya
shilingi milioni 400, lakini kitendo cha Etoile kukiuka kipengele kimoja cha
mkataba, nyota huyu aliwamaliza.
Timu hii haikumlipa mshahara kwa miezi mitatu kama
takwa la kimkataba, lakini iliwahi kuelezwa kuwa Etoile walifanya hivyo kama
sehemu ya adhabu kwa Okwi kwani alikaa muda mrefu bila kurudi kambini baada ya
kuruhusiwa kuichezea timu ya Taifa ya Uganda.
Okwi alipeleka kesi FIFA akipambana na Etoile.
Simba nao walikuwa wanapambana na Etoile ili walipwa fedhe zao za usajili.
FIFA baada ya kuona Okwi amekaa muda mrefu bila
kucheza, walimpa ruhusa ya kucheza kwa muda wa miezi sita katika Sport Club
Villa ya Uganda ili kulinda kiwango chake wakati kesi yake inasubiriwa.
Villa walimuuza Okwi kwenda klabu ya Yanga na
mengi yakaibuka juu ya suala hilo. Kumbe Okwi alikuwa na haki kwasababu
hakutekelezewa kipengele cha mkataba na akawa mchezaji huru na ndio maana
majogoo wa Kampala walimuuza.
Suala hili linafanana na la Abdi Banda kwa kiasi Fulani.
Coastal wanadai kinda huyu alikataa kuchukua mshahara baada ya kurubuniwa na
watu, lakini kiukweli ni nani atakwepa kuchukua mshahara wake?
Baadaye mkataba ukavunjika kwa kushindwa kumlipa
mshahara wa miezi mitatu mfululizo na akawa mchezaji huru.
Ukifuatilia sakata la Okwi na Banda, Simba haikuwa
na tatizo na Yanga wala Coastal Union, bali wachezaji walikuwa na matatizo na
tmu zao.
Kwa namna Simba walivyoweza kutafsiri sheria za
kimkataba za wachezaji hawa na kuona ni sahihi kuwasajili, nadhani mwenyekiti
wa kamati ya Usajili YA Simba, Zacharia Hans Poppe amewapiga bao wapinzani.
Alijiamini wakati wa usajili huu kwasababu
wanasheria waliweza kumtafsiria vizuri mikataba ya wachezaji hawa na kuona
imevunjika kisheria.
Kwa hapa Hans Poppe amefanikiwa kuwa makini na
hatimaye ameibuka mshindi.
Lakini kwa viongozi wa Yanga na Coastal Union
wamechemsha kwa hili. Najua sio wao tu, wapo wengine wenye ueledi mdogo juu
masuala ya kisheria.
Hata kama Yanga watakwenda CAF au FIFA au mahakama
ya Rufani ya juu ya michezo, sidhani kama itakuwa rahisi kushinda kama
walikiuka kipengele cha 8 cha mkataba.
FIFA watakuwa na majibu yale yale kama ya kamati
ya Sheria na Hadhi za wachezaji. Rejea Okwi na Etoile Du Sahel.
Labda suala la kuongea na klabu ya Misri na
kufikia makubiliano bila ruhusa ya Yanga linaweza kuwa la msingi kwa sasa.
Hapa kuna hoja ya Msingi kama kweli jambo hili
lilitokea. Ni marufuka kuongea na mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine bila
ruhusu ya timu inayommiliki.
Viongozi wa mpira wa miguu nchini, jifunzeni
kuheshimu vipengele vya mikataba ya wachezaji.